Ili Serikali ya awamu ya sita itimize azma yake ya Tanzania
kuilisha dunia, wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo wanamchango mkubwa katika
kufanikisha azma hiyo, pamoja na Serikali kuwa na mipango thabiti ya matumizi
ya mbegu zilizoboreshwa na teknolojia ya kisasa katika kilimo.
Katika kilimo mbegu ni muhimu kutokana na ukweli kwamba mbegu
ni chanzo cha uhai, ni chanzo cha nishati, chanzo cha chakula na dawa, pia
mbegu ni chanzo cha malighafi za viwandani na vilevile ni chanzo cha mapato ya
fedha za kigeni.
Katika kuzingatia suala la mbegu ni muhimu kuwa na mbegu
zilizoboreshwa ili kupata mavuno ya kutosha na kukabiliana na magonjwa, wadudu
waharibifu, ukame, magungu pamoja na changamoto zingine za mazingira yakiwamo
mabadiliko ya tabia nchi.
Serikali katika kutambua umuhimu wa mbegu zilizoboreshwa hadi
sasa nchini kuna Wakala wa Mbegu za Kilomo (ASA), inayohusika na utafiti,
ubunifu, pia uzalishaji mbegu nchini.
Pia kuna Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI)
iliyoanzishwa mwaka 2003, ikiwa na jukumu la kuthibitisha na kukuza mbegu bora
zinazozalishwa nchini ama kuingizwa kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kuuzwa.
Katika kutambua umuhimu wa kilimo kwa bara la Afrika
aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Hayati Kofi Annan alianzisha Taasisi inayojishughulisha
na ukuzaji wa kilimo Afrika (AGRA) mwaka 2006, ili kuboresha maisha ya wakulima
wadogo wa Afrika wanaohangaika na kilimo cha kujikimu na kuwafanya walime
kilimo cha biashara.
Maono hayo ya Muasisi wa AGRA Hayati Annan, yameigusa
Tanzania kupitia taasisi hiyo iliyopo kwenye mataifa kadhaa ya Afrika, ikishirikiana
na Serikali, Wadau wa kilimo na Wakulima katika kuhamasisha kilimo cha kisasa,
matumizi ya mbegu zilizoboreshwa pamoja na kuwa na soko la chakula lenye ushindani
Afrika.
Afisa wa Programu ya Mifumo ya Mbegu AGRA, Ipyana Mwakasaka amesema
taasisi hiyo imesaidia katika kuwawezesha watafiti nchini kubuni na kuja na
aina mbalimbali za mbegu karibu 44 za mazao mbalimbali kama vile mahindi, mpunga,
maharage soya, mihogo na mengineyo.
“Kati ya mbegu hizo 44 ambazo AGRA imewasaidia watafiti
kufanya tafiti na kubuni mbegu, aina 30 ya mbegu hizo zimeshaingia sokoni baada
ya kuidhinishwa na waziri mwenye dhamana ya kilimo, na zinafanyakazi vizuri
katika mikoa mbalimbali,” alisema Bw. Mwakasaka.
Amesema kwamba AGRA pia imesaidia kuanzisha na kuyaimarisha
makampuni 15 ya mbegu ya ndani ya nchi, katika kusaidia mkakati wa Serikali wa
kuzalisha asilimia 75 ya mbegu nchini ili kuepukana na athari za kutegemea mbegu
kutoka nje ya nchi.
“Kampuni hizo binafsi 15 za uzalisahji mbegu zilizopata
msaada wa AGRA zimefanikiwa kuzalisha mbegu zenye ubora wa hali ya juu zinazofikia
ujazo wa tani mitamraba 35,000,” alisema Bw. Mwakasaka na kuongeza “Uzalishaji
wa mbegu bora umeongezeka kutoka tani 36,614 mwaka 2015 hadi kufikia tani
71,000 mwaka 2020.”
Bw. Mwakasaka amesema kwamba kumekuwapo pia na mafanikio ya
kuongezeka kwa uzalishaji wa mbegu nchini kutoka chini ya asilimia 20 mwaka 2006
hadi kufikia uzalishaji wa mbegu unaozidi zaidi ya asilimia 60 kwa sasa.
Katika kukabiliana na upungufu wa Maafisa Ugani, AGRA imetoa
mafunzo kwa wakulima viongozi 5000 wanaowahudumia wakulima wapatao 100-200, kwa
kusaidiana na Maafisa Ugani Kata katika kupeleka taarifa za kilimo kwa
wakulima.
AGRA pia inahusika katika kusaidia sera za pamoja na
mazingira bora ya kilimo nchini kwa kufanikisha kuandikishwa Serikalini kwa
mbegu za aina mbalimbali zilizoboreshwa pamoja na kuondoa ada ya uandikishaji.
Licha ya mafanikio hayo bado Tanzania inakabiliwa na
changamoto ya upungufu wa mbegu zilizoboreshwa, pamoja na kuzalisha asilimia 60,
kuna asilimia 40 nchi inaagiza nje ya nchi hususan kwenye mbegu za mahindi,
lakini kwenye mazao mengine ni zaidi ya asilimia 90.
Changamoto hiyo pia inaeelezwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa
Chama cha Wafanyabiashara ya Mbegu Tanzania (TASTA), Bw. Bob Baldwin Shuma ambaye
amesema asilimia kubwa ya mbegu za hybrid zinazotumika nchini zinazalishwa
kutoka nje ya nchi.
“Mbegu zote za hybrid zinazoletwa kutoka nje haziji tu na
wala sio msaada, bali zinanunuliwa kwa fedha za kigeni ndipo mnunuzi aende kununua
kama ni Zimbabwe ama Zambia,” alisema Bw. Shuma na kuongeza, “Bado inatakiwa
kulipa kodi kadhaa na ndio maana zinauzwa bei ghali, lakini kwa mfano sasa
kunauhaba wa dola tafsiri yake ni nini tutakapo kosa dola mbegu zitakosekana,
kama hatuzalishi mbegu sisi wenyewe za kutosha kunahatari”.
Amesema amekuwa akijitahidi sana kusaidia kuhakikisha
kunakuwa na Sera nzuri, kwani ardhi zipo tena safi, kwa mfano maeneo
yatakayotengwa kwa irrigation (kilimo cha umwagiliaji) mbegu za hybrid
zizalishwe huko huko.
“Tuna mabonde mazuri ambayo yamezungumzwa yapo, hayo mabonde
mimi nina nia ya kuyataja tuyafanya yawe chini ya Serikali lakini yatolewe kwa
ajili ya kuzalishia mbegu za hybrid kwa njia ya umwagiliaji,” alisema Bw.
Shuma.
Ameeleza kwamba ili kuzalisha mbegu za hybrid sheria ya
TOSCI inasema kuzalisha mbegu hizo unatakiwa kuwa na nafasi ya mita 400 huku na
mita 400 huku na mtu mwingine asilime mahindi katika eneo hilo.
“Kwa hiyo ardhi tulionayo lazima tuwe za Sera nzuri, kule
tunapoenda kununua mbegu za hybrid wamefanya hivyo, sisi tusipofanya hivyo
tutaendelea kununua huko mbegu hizo,” alisema Bw. Shuma.
Pamoja na changamoto za upungufu wa mbegu mabadiliko ya
tabia nchi nayo yameelezwa kuwa yamekuwa yakichangia kuangamiza mbegu nyingi za
asili nchini, kutokana na mbegu hizo kushindwa kuhimili changamoto zinazotokana
na mabadiliko hayo.
Akiongelea suala hilo Afisa wa Taasisi ya Agri experience Dk.
Emmarold Mneney, ameelezea changamoto za mabadiliko ya tabia nchi yanayopelekea
kutokea kwa ukame, mafuriko, joto kali, kuibuka kwa magonjwa mapya na wadudu
wapya yanavyoathiri mbegu za asili.
“Kumekuwa na dhana potofu kuwa mbegu zilizoboreshwa
zinatumika kupoteza mbegu za asili, ukweli ni kwamba mbegu za asili
zinaathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi,” alisema Dk. Mneney na kuongeza
“Mbegu nyingi za asili zinashindwa kuhimili hali ya mafuriko, mvua chache
pamoja na joto kali, hapo ndipo mbegu zilizoboreshwa zinapokuja kusaidia”.
Dk. Mneney amesema wanachofanya watafiki wanaozalisha mbegu
zilizoboreshwa ni kurudi katika mbegu za asili kuzizidishia nguvu ili ziweze
kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.
Akielezea historia ya tafiti za mbegu duniani, Dk. Mneney
amesema utafiti ndio uliosaidia kupatikana kwa mbegu ya mahindi, kutoka kwenye Mexican
grass (majani ya Mexico) na kuboreshwa kuwa mahindi tunayokula leo.
“Leo tusinge kuwa tunakula mahindi kusinge kuwa na utafiti
wa mbegu, kwani mahindi yemetokana na tafiti iliyofanywa kutoka kwenye Mexican
grass (majani ya Mexico) kwenye karne ya 16,” alisema Dk. Mneney.
Dk. Mneney amesema mbegu zilizoboreshwa ni ufumbuzi ambao
utaendelea kuwapo duniani katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja
na kuboresha uzalishaji wa mazao ili kuendana na wakati.
Pamoja na mambo mengine, Dk. Mneney amesema mafanikio ya
azma ya Tanzania kuilisha dunia yatafikiwa iwapo tu Serikali itaongeza bajeti
ya kilimo na kuwekeza zaidi kwenye tafiti za uzalishaji wa mbegu
zilizoboreshwa.
0 Maoni