WAZIRI MKUU Mhe. Kassim
Majaliwa amesema wanafunzi 1,206,995 kati ya 1,397,370 waliohitimu darasa la
saba mwaka huu wanatarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza ifikapo Januari,
mwakani.
“Wanafunzi 1,206,995 sawa na
asilimia 86.4 ya wanafunzi 1,397,370 waliosajiliwa kufanya mtihani wa kuhitimu
elimu ya msingi mwaka 2023 wanatarajiwa kujiunga na elimu ya sekondari Januari,
2024,” amesema Mhe. Majaliwa.
Hayo yamesemwa jana (Ijumaa,
Novemba 10, 2023) na Waziri Mkuu wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 13
wa Bunge jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Januari 30, mwakani.
Waziri Mkuu amesema Serikali
inaendelea kukamilisha maandalizi muhimu ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha
kwanza mwaka 2024 ikiwemo ujenzi wa miundombinu. “Nitumie fursa hii
kuwakumbusha Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa wote nchini wahakikishe kuwa ujenzi wa
miundombinu yote katika shule za sekondari unakamilika kabla ya tarehe 30
Novemba, 2023.”
Amesema Serikali
itawachukulia hatua wote watakaoshindwa kukamilisha ujenzi wa miundombinu
katika shule za sekondari. “Wakuu wa Mikoa fanyeni ufuatiliaji, Serikali
imeshapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi katika Halmashauri zote nchini hivyo
hakuna sababu wala visingizio vya kutokamilisha ujenzi kwa wakati,”
amesisitiza.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu
amesema Serikali inatarajia kuandikisha watoto wa elimu ya awali 1,877,484
wenye rika lengwa wakiwemo wavulana 934,560 na wasichana 942,924 na darasa la
kwanza 1,729,180 wakiwemo wavulana 860,870 na wasichana 868,310 ifikapo
Januari, 2024.
“Hadi sasa jumla ya watoto
wa elimu ya awali 407,138 sawa na asilimia 21.7 wakiwemo wavulana 201,244 na
wasichana 206,253 wameandikishwa. Kati ya watoto wa elimu ya awali, wenye
mahitaji maalum walioandikishwa ni 960 kati yao wavulana ni 488 na wasichana ni
472.”
Amesema walioandikishwa
kujiunga darasa la kwanza ni 593,452 sawa na asilimia 34.3 wakiwemo wavulana
293,728 na wasichana 299,724. “Kati ya wanafunzi wa darasa la kwanza
walioandikishwa wenye mahitaji maalum ni 1,365 wakiwemo wavulana ni 733 na
wasichana 632,” amesema.
Amewaagiza Wakuu wa Mikoa
yote nchini wasimamie zoezi la uandikishaji katika maeneo yao jambo ambalo
amesema itakuwa vema likihitimishwa Desemba 31, mwaka huu. “Nitumie fursa hii
pia kuwakumbusha wazazi na walezi wote wenye watoto wenye rika lengwa,
wawaandikishe watoto hao ili waweze kuanza masomo ifikapo Januari, 2024.”
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu Majaliwa amesema kutokana na jitihada za Serikali za kuimarisha
upatikanaji wa pembejeo zikiwemo mbolea, hadi Oktoba 31, mwaka huu wakulima
zaidi ya milioni 3.6 walikuwa wamesajiliwa na kupata namba za utambulisho za
kununua mbolea ya ruzuku.
“Nitumie fursa hii
kuwaelekeza Wakuu wa Wilaya ambao pia ni Wenyeviti wa Kamati za Pembejeo za
Wilaya wawahamasishe wakulima kujisajili na kutoa taarifa sahihi kuhusu mazao
wanayolima na ukubwa wa mashamba yao kwenye madaftari ya wakulima ambayo
yamesambazwa kwa watendaji wa vijiji na mitaa ili taarifa zao ziweze kuingizwa
kwenye mfumo na wapatiwe namba za kununulia mbolea ya ruzuku.”
Ameitaka Wizara ya Kilimo
ihakikishe mbolea inapatikana kwa wakati na ishirikiane na Wakuu wa Wilaya
kusimamia kwa karibu usambazaji wa mbolea kwa wakulima. “Hatua hii iende
sambamba na kutatua changamoto zinazojitokeza wakati wa usambazaji wa pembejeo
hiyo muhimu,” amesisitiza.
Amezitaka kampuni na taasisi
zinazozalisha mbegu bora ziongeze kiwango cha uzalishaji na kuweka utaratibu
mahsusi wa kufikisha mbegu hizo kwa wakulima katika maeneo yao ya uzalishaji.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni