Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam,
Mhe. Albert Chalamila amefanya Mkutano mkubwa wa kusikiliza na kutatua kero za
wananchi wa Singiziwa-Chanika jijini Dar es Salaam ambapo amesikiliza kero na
kuzipatia majawabu hadi usiku.
RC Chalamila akisikiliza
kero mbalimbali zinazowakabili wananchi hao amekemea tabia ovu za vijana
maarufu kwa jina la Panya Road, ambazo zinahatarisha maisha ya watu na
kuwafanya kuishi kwa wasiwasi.
Wakati akizungumza kwenye
mkutano huo jana amesema hao vijana wamekuwa tishio kwa usalama wa
wananchi na mali zao hivyo kutakuwa na oparesheni maalum itakayofanyika baadhi
ya maeneo ambayo vijana hao hatari hutumia kama "maskani" yao lengo
likiwa ni kujenga Dar es salaam na Tanzania yenye amani.
"Kutakuwa na oparesheni
maalum ambayo itapita kwenye baadhi ya maeneo ambayo tunajua ndio maskani ya
panyaroad iliwahi kutokea vingunguti alikuwa kibaka mmoja ambaye tulikuwa
tunamuita panyaroad mwandamizi alipouliwa wenzake wakatoka huku Chanika
wakaenda kufanya fujo Vingunguti kwanini mwandamizi wetu ameuliwa lakini
nashukuru sana Mungu kama mapambio waliyaimba vizuri," alisema Mhe
Chalamila.
Akiendelea kusikiliza kero
mbalimbali za wananchi hao Mhe. Chalamila alibaini matatizo makubwa
yanayowakabili wananchi hao zikiwemo barabara, shule, huduma mbaya vituo vya
afya, maji, umeme, migogoro ya ardhi, mwongozo wa soko la wamachinga, matatizo
kijamii na familia huku RC Chalamila akibaini uwepo wa vitendo vya kikatili
wanavyokumbana navyo watoto, ushoga na madanguro.
Aidha, wananchi hao
walimuomba Mkuu wa Mkoa huyo kuwasaidia kutatua kero zao sababu ni muda mrefu
wanahangaika, ambapo baada ya kusikiliza kero hizo aliwataka viongozi wenye
mamlaka na idara husika kujibu kero hizo sababu lengo ni kupata ufumbuzi wa
kila kero.
Wakiongozwa na mkuu wa
wilaya ya Ilala Mhe Edward J Mpogolo viongozi hao walitoa majibu ya baadhi kero
na kuahidi kushughulikia na kutatua kero zilizohitaji ufuatiliaji zaidi
Kwa kumalizia Mhe Chalamila
alisema matatizo na alitoa rai kwa viongozi kutembelea maeneo yao mara kwa
kuepuka matatizo kuwa sugu, na aliwaasa wazazi wawe makini na makuzi ya watoto
kuepuka taifa lenye vijana na viongozi wasiojielewa hapo badae ikiwa
watajiingiza kwenye makundi ya panya road au ushoga.
0 Maoni