Mkuu wa mkoa wa Dar es
salaam Mhe Albert Chalamila akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe
Edward Mpogolo leo Novemba 8,2023 amefanya ziara kwa treni za mjini kutoka
stesheni ya Kamata kwenda Pugu kuona adha wanazokumbana nazo abiria.
Mhe Albert Chalamila
alitumia usafiri huo ili kuweza kuwasikiliza abiria na kuona kero na changamoto
wanazokumbana nazo abiria na aliwaeleza kuwa mhe Rais Dkt Samia S. Hassan
amewaona jinsi walivyodandia na kuning'inia kwenye treni hivyo amemuagiza afuatilie
kujua ukweli wa Changamoto hiyo.
Aidha Abiria waliokua
wakitumia usafiri huo walitumia fursa hiyo kumwelezea RC kero zao zikiwemo
matumizi mabaya ya tiketi na ukataji wake, kutokuwepo usimamizi mzuri kwenye
mabehewa ya wanafunzi na wazee, kuboreshwa huduma za vyoo, kukosa vituo vya
kujikinga na mvua au jua, na wengine waliomba kuongezewa siku ya jumamosi
wapate huduma za treni sababu pilikapilika bado nyingi na pia kuboreshwe geti
la kutokea pale Kamata.
Hata hivyo RC Chalamila
alisema changamoto hizo kwa sehemu kubwa zitatatuliwa hivyo ameaidi kuendelea
kuzitatua na pia kufanya ziara za kushtukiza na za taarifa ili kuwasaidia
wananchi.
Pia Mhe Chalamila amemtaka
mkandarasi anayejenga barabara ya Pugu ajenge barabara za kando kuepuka
wananchi kukwama kwenye foleni na kusababisha watu kuchelewa kazini,
"Kipande cha kutoka Banana mpaka mitaa ya Ukonga, magari mengi yanapita
kwenye njia moja kwahiyo tumekubaliana mchina aongeze barabara ili magari
yaweze kupishana," alisema.
Kwa upande wa Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Amina Lumuli aliwaahidi abiria wanaendelea
kutatua changamoto wanazopata na hadi sasa washaongeza 'ruti' na kufikia 8
hivyo abiria watasafiri kwa wakati na salama kufika kwenye shughuli zao au
makwao, na alitoa wito kwa wananchi wote wafuate sheria na taratibu usafiri
huo.
0 Maoni