Naibu Waziri Mkuu na Waziri
wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha kuwa wanatekeleza agizo la Rais,
Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuendelea kutoa elimu ya mlipakodi kwa Watanzania
na Wafanyabiashara ili kuleta ufanisi katika ukusanyaji kodi, kuendelea kuweka
uhusiano mzuri kati ya Wafanyabiashara na TRA na kuhakikisha kuwa kila
anayestahili kulipa kodi nchini, anailipa bila misukosuko.
Dkt. Biteko amesema hayo
wakati alipokuwa mgeni rasmi katika Sherehe ya utoaji Tuzo kwa Walipakodi Bora
kwa mwaka 2022/2023 iliyofanyika jana 24 Novemba, 2023 Jijini Dar es Salaam.
“Wafanyabiashara wanapaswa
kulelewa ili walipe kodi zaidi, wanapaswa kufundishwa umuhimu wa kulipa kodi,
na kazi hii ni ya kwenu Wizara ya Fedha na TRA na ninafurahi kwamba mnaifanya
vizuri, sisi tunawatakia kila la heri katika kuifanya kazi hiyo ili mchango wa
walipa kodi uendelee kuwa mkubwa ili tuweze kufikia malengo tunayojiwekea.”
Alisema Dkt. Biteko
Alieleza kuwa, Serikali ya
Awamu Sita itaendelea kufungua nchi ili kuvutia uwekezaji zaidi, kuweka
mazingira rafiki ya uwekezaji, pamoja na kupambana na kutokomeza rushwa ikiwemo
kwenye sehemu zinazohusisha Wafanyabiashara.
Dkt. Biteko aliipongeza TRA
kwa kusimamia vizuri zoezi la ukusanyaji mapato nchini akitolea mfano malengo
waliyowekewa mwaka 2022/23 ambayo wameyafikia kwa asilimia 97.4 kwani
walikusanya shilingi Trilioni 24.11 kati ya shilingi Trilioni 24.76
walizopangiwa na kueleza kuwa hiyo si hatua ndogo hivyo TRA na Walipakodi wote
wanastahili pongezi.
Aidha, Dkt. Biteko ametaka
Wafanyabiashara watambue kuwa, kazi ya kujenga nchi si ya Serikali pekeyake
bali ni ya watanzania wote hivyo amewataka kuendelea kulipa kodi ili zikajenge
nchi kwa namna mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Barabara, Shule, Umeme, Maji,
Hospitali zenye madawa na nyenzo nyingine ambazo uwepo wake unahitaji fedha.
Dkt. Biteko alitoa pongezi
kwa Wizara ya Fedha pamoja na TRA kwa kuandaa shughuli hiyo muhimu ya
kuwatambua Walipakodi na kuwapa Tuzo kama kielelezo cha kuonyesha umuhimu wao
kwa uchumi wa Tanzania.
Aliwapongeza pia
Wafanyabiashara waliopata Tuzo katika sherehe hiyo huku akieleza kuwa, kwa wale
waliokosa Serikali bado inatambua mchango wao na waone kuwa Tuzo hizo ni
motisha kwao ya kuchangamkia fursa ya kutambuliwa.
Washindi wa Kitaifa katika
Tuzo hizo za Walipakodi Bora kwa mwaka 2022/2023 ni Benki ya CRDB (mshindi wa
Tatu), Tanzania Breweries (Mshindi wa Pili), huku Mshindi wa kwanza akiwa ni
Benki ya NMB.
Viongozi mbalimbali
waliohudhuria sherehe hiyo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Mipango na
Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Chande,
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, Katibu Mkuu, Wizara ya
Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata na
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), Yusuph Mwenda.
0 Maoni