Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali
ya Taifa Muhimbili (MNH) Prof. Mohamed Janabi amesema hospitali hiyo itaendelea
kuimarisha huduma bora kwa mteja ili kuwavutia watu wengi ndani na nje ya nchi
kuja kutibiwa Muhimbili.
Prof. Janabi amaeyasema
hayo alipokua akizungumza mbele ya Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel
alipotembelea Muhimbili a kufanya kikao na wakuu wa Taasisi za afya ikiwemo
MNH, JKCI, MOI, MSD, NHIF, TMDA, Mganga Mkuu wa Mkoa pamoja na Waganga Wafawidhi wa
Hospitali za Rufaa za mkoa wa Dar es Saalam.
Prof. Janabi amesema tofauti
kubwa iliyopo katika Hospitali za Umma kwa sasa ni suala la huduma bora kwa
mteja kwani serikali imewezesha kuwepo kwa vifaa tiba vya kisasa vyenye ubora
hali ya juu na wataalamu hivyo hatuna budi kuzingatia suala la kutoa huduma
bora kwa mteja.
Akielezea mafanikio ya
Muhimbili amesema chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita MNH, imeendelea
kutoa huduma za kibingwa na kibobezi ambapo hivi karibuni kwa upande wa
Muhimbili Mloganzila jumla ya wagonjwa 7 wamepandikizwa figo na mwishoni mwa
mwezi huu itaweka kambi maalumu ya kupandikiza nyonga na magoti kwa wagonjwa
wenye changamoto hizo.
Aidha, Prof. Janabi ametumia
fursa hiyo kuwataka wananchi kujiunga na bima ya afya kabla hawajaumwa kwakua
matibabu ni gharama na kusisitiza kuwa huduma za afya zinapaswa kuchangiwa ili
kuwa endelevu.
0 Maoni