Naibu Waziri Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe Ridhiwani Kikwete
ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Iringa kwa usimamizi mzuri katika utekelezaji wa
miradi inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii -TASAF.
Amesema kupitia usimamizi
mzuri wa utelekezaji wa miradi hiyo, TASAF imeweza kutatua changamoto
mbalimbali za kiuchumi na kijamii katika kaya za walengwa pamoja na wananchi
katika maeneo ya utekelezaji.
Mhe. Ridhiwani amesema hayo
mkoani Iringa wakati akizungumza na Walengwa wa Tasaf wa Kata ya Ruaha iliyopo
katika Manispaa ya Iringa, mara baada ya kukagua daraja lilojengwa katika eneo
la Kingemgosi ikiwa ni utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya
Masikini unaotekelezwa na TASAF.
Kwa mujibu wa taarifa ya
TASAF mkoa wa Iringa inaonesha kuwa jumla ya miradi 474 ikiwemo uchimbaji wa
visima vya asili, utengenezaji wa barabara, uzibaji wa makorongo na kuanzishwa
kwa mashamba ya korosho ilitekelezwa kati ya Julai 2022 na Juni 2023.
Pia, mkoa ulipokea jumla ya shilingi
bilioni 10.3, kati ya hizo shilingi bilioni 8.9 zilitolewa kwa Walengwa 30,988
kutoka vijiji 585 wakati shilingi bilioni 21.6 zilikuwa ni kwa ajili ya
usimamizi ngazi ya mkoa na halmashauri.
“Nimefarijika sana kwa namna
shughuli za TASAF zinavofanyika hapa katika mkoa wa Iringa likiwemo daraja
lililojengwa katika eneo la Kigenamgosi, haya ni matokeo ya ushirikiano thabiti
kati ya uongozi wa mkoa na watendaji wote wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii,”
amesema.
Kwa upande wake, Mwakilishi
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Oscar Maduhu amewahakikishia na walengwa wa TASAF
kuwa waendelea kubuni miradi ya kimaendeleo kwani serikali imetanga jumla ya
Sh. 51 bilioni kwa ajili ya Walengwa hao.
“TASAF inaendelea kuhakikisha walengwa wote
wanahudumiwa ipasavyo ili kuwaondoa katika hali ya umasikini uliokithiri
kupitia ruzuku, miradi ya ajira za muda pamoja na kuwapa elimu ya kuweka na
kukopa katika vikundi mbalimbali,” alisema Maduhu.
Awali, Mkuu wa wilaya ya
Iringa Mjini, Mhe. Veronika Kessy amesema mpango wa TASAF umesaidia kuinua hali
za uchumi kwa walengwa pamoja na kuchechemua biashara mbalimbali kwa wananchi
wenye kipato cha chini.
Amesema, utoaji fedha za
Mpango umewezesha kaya za walengwa kuboresha makazi na kujenga nyumba za
matofali ya kuchoma na kuezeka kwa bati badala ya nyasi.
“Hadi kufikia mwezi Juni
2023, jumla ya walengwa 918 wa TASAF katika mkoa wa Iringa waliweza kuboresha
makazi yao,” amesema.
Na. Lusungu Helela- Iringa
0 Maoni