Katibu Mkuu wa Chama Cha
Mapinduzi, Ndugu Daniel Godfrey Chongolo amesema kupitia utekelezaji wa Ilani
yake ya Uchaguzi ya 2020 – 2025, CCM itahakikisha Serikali inaendelea kuweka
mazingira bora na kuwajengea uwezo makandarasi na washauri waelekezi wazawa,
ili waweze kutekeleza miradi mingi na mikubwa ndani ya nchi na hata kushindana
nje ya Tanzania, ikiwemo kulipwa madeni yao na kuwahishiwa malipo ya kazi
katika miradi wanayotekeleza.
Ndugu Chongolo amesema hatua
ya kuwatumia wakandarasi na washauri waelekezi wazalendo wa Kitanzania katika
miradi hiyo mbalimbali ya ujenzi itaokoa fedha nyingi, ambazo kwa sasa
zinalipwa kwa makandarasi wa nje, hivyo zitabakia katika mzunguko wa fedha na
uchumi ndani ya nchi, zitaongeza kipato kwa wahusika, huku pia wakipata nafasi
ya kuongeza ujuzi na kutengeneza fursa za ajira kwa Watanzania.
Mbali ya kuwataka watendaji
wa Serikali, hususan katika Wizara ya Ujenzi kuacha mitazamo hasi dhidi ya
wakandarasi na wahandisi wazawa kuwa hawawezi kazi, pia amewataka baadhi ya
makandarasi wa ndani nao kuacha kuichafua tasnia ya ujenzi, kwa kuwa na kampuni
za mfukoni (briefcase company), ambazo hazina uwezo wa kufanya kazi, hali
ambayo inajenga na kuhalalisha dhana kuwa kuna wazawa wanafanya utapeli kwa
kutumia taaluma hiyo.
Katibu Mkuu Ndugu Chongolo
amesema hayo jana Jumanne, Novemba 21, 2023, wakati akitoa salaam za Chama Cha
Mapinduzi kwenye Mkutano wa Makandarasi na Washauri Waelekezi Wazawa,
uliofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention, jijini Dodoma, ambapo
amewaambia kuwa CCM inatambua changamoto zote zinazowasibu, likiwemo suala la
madeni wanayodai na kucheleweshewa malipo yao katika miradi anuai
wanayotekeleza maeneo mbalimbali nchini.
“Mkutano huu ni muhimu sana.
Jana nimekaa na mawaziri wote wawili hawa, Waziri wa Ujenzi na Waziri wa Fedha
hadi usiku wa manane, ilibidi tukae kwa muda mrefu sana. Nilitaka kwanza kujua
masuala kadhaa kabla sijaja hapa leo. Na hasa nililowaita na kuzungumza nao ni
kuhusu malipo yenu. Nina uhakika hapa tukisema tupitishe karatasi kila mtu
aandike changamoto yake, jambo la kwanza kila mmoja litakuwa ni malipo, malipo,
malipo.
“Wamenieleza kwa kina jinsi
wanavyochukua hatua kadhaa, hasa kutekeleza maelekezo na maagizo ya Mhe. Rais
Dokta Samia Suluhu Hassan amewaagiza kuhakikisha wanafanya msawazo wa malipo ya
madeni ya wakandarasi na pia kila mkandarasi alipwe anapo-raise certificate.
Pia labda niseme hapa, ni muhimu mkaenda pia kujifunza kwa wenzenu wa REA
(Wakala wa Umeme Vijijini) ili utaratibu ule wanaotumia kulipa wakandarasi wa
umeme, uweze kutumika pia huku Ujenzi. Kule hakuna malalamiko sana,” amesema
Katibu Mkuu Chongolo.
Pamoja na kuipongeza
Serikali kwa kufanya mabadiliko ya Sheria ya Manunuzi, iliyopandisha kiwango cha
thamani ya miradi inayoweza kutekelezwa na wakandarasi wa ndani, kutoka mradi
wa thamani ya Tsh. 10 bilioni, hadi kufikia mradi wa Tsh. 50 bilioni, Katibu
Mkuu Ndugu Chongolo ameitaka Serikali, kupitia Wizara ya Ujenzi na Wizara ya
Fedha, kuweka utaratibu wa kisheria ambao utakaolazimu ushirikishwaji wa
makandarasi wazawa katika miradi yote mikubwa nchini.
“Hili la ushirikishwaji
kwenye miradi mikubwa ya kimkakati kama SGR, Bwawa la Mwalimu Nyerere, hili
tunaweza kulimaliza kwa kuweka sheria ya kulazimisha wakandarasi wakubwa
wanapoomba miradi hapa kwetu basi waje na wakandarasi wa ndani kama ilivyo kwa
Washauri Majenzi yaani consultants. Hii
pia ni nzuri kwa maslahi mapana ya nchi yetu.
“Mfano tunafanya mradi
mkubwa wa SGR lakini mkandarasi akimaliza akiondoka siku tukitaka kufanya ‘ka
extension kadogo hata ka kilometa moja, hatutaweza kwa sababu hatukuweka
wakandarasi wetu wapate ujuzi. Ni
kupitia watu wetu kushiriki, ndiyo tungeweza kufanya kama ambavyo baadhi ya
nchi zingine duniani zinafanya kujenga uwezo kwa watu wao kwa kitu kinachoitwa
‘Technological Transfer’,” amesema Katibu Mkuu Chongolo.
Ndugu Chongolo
amewahakikishia Makandarasi na Washauri Waelekezi hao wa ndani kuwa CCM
itasimamia maslahi yao, kwa kadri ambavyo Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka
2020 – 2025 ilivyoahidi kuwa Chama kitaielekeza Serikali kuhakikisha inaweka
mazingira rafiki na bora, ikiwa ni pamoja na kujengewa uwezo wa kupata kazi
nyingi zaidi za fedha za Mfuko wa Barabara na kuwawazesha kupata mikopo ili
washiriki kikamilifu kwenye miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara, madaraja,
majengo, maji na mingine mingi.
Katibu Mkuu Chongolo pia
aliwataka wazawa hao kutanguliza mbele weledi, uaminifu, kujali rasilimali watu
na thamani ya fedha wanapofanikiwa kupata miradi hiyo ya Serikali inayotumia
fedha za umma, huku akitoa wito kuwataka waache ubinafsi wa kila mtu kupambana
mmoja mmoja katika kutafuta miradi, badala yake watambue umuhimu wa kuungana
(Joint Ventures), na wafanye hivyo mapema, si wakati wa kutafuta miradi pekee,
ili kujenga kuaminiana katika ubia wa kibiashara wanaokuwa wameingia.
0 Maoni