WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ameitaka Wizara ya Fedha iimarishe mifumo ya kuwalinda watumiaji wa huduma za
fedha ili baadhi ya watoa huduma wasio waadilifu wasitumie changamoto ya uelewa
mdogo wa masuala ya fedha kwa baadhi ya wananchi na kuwadhulumu.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa
amesema Wizara ya Fedha iendelee kushirikiana na na watoa huduma za fedha kutoa
elimu kwa wananchi katika maeneo muhimu yakiwemo ya usimamizi wa fedha binafsi,
kuweka akiba, mikopo, uwekezaji kupitia hatifungani na hisa, bima, mpango wa
kujiandaa na maisha ya uzeeni pamoja na kodi.
“Wizara ya Fedha iandae
mpango maalumu wa kutoa hamasa kwa Watanzania ili wajenge utamaduni wa kutumia
huduma rasmi za kifedha, pia elimu iendelee kutolewa kuhusu wajibu wa kila
mmoja kudai na kutoa risiti kwa malipo yanayofanyika.”
Ametoa maagizo hayo leo
(Jumatano, Novemba 22, 2023) alipofungua Wiki ya Huduma ya Fedha Kitaifa,
jijini Arusha, ambapo ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa watoa huduma za
kifedha wapunguze gharama za upatikanaji wa huduma za fedha zikiwemo riba na
ada ili wananchi wengi watumie huduma za fedha zilizo rasmi.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa
ameisisitiza Wizara ya Fedha iendelee kusimamia na kuratibu utekelezaji wa
Programu ya kutoa elimu ya fedha kwa umma na kuhakikisha kuwa elimu hiyo
inawafikia wananchi wengi zaidi mijini na vijijini.
Waziri Mkuu amesema Wizara
ya Fedha inatakiwa iandae mpango maalumu wa kutoa hamasa kwa Watanzania ili
wajenge utamaduni wa kutumia huduma rasmi za kifedha pamoja na kuratibu gharama
za huduma za fedha. “Pia, elimu iendelee kutolewa kuhusu wajibu wa kila mmoja
kudai na kutoa risiti kwa malipo yanayofanyika.
Waziri Mkuu amesema watoa
huduma za kifedha hawana budi kujenga uelewa wa kutosha kwa wananchi kabla ya
kufunga nao mikataba, pamoja na kuwafafanulia taratibu na masharti yao kabla
hawajatoa kwao huduma hizo za fedha. Pia amewataka watoa huduma hao waweke
mkakati mahususi wa kuongeza matumizi huduma kwa njia ya kidijitali pamoja na
kuzisogeza hadi maeneo ya pembezoni na vijijini ili wananchi walio wengi
wanufaike.
“Watoa huduma za fedha
ongezeni ubunifu katika utoaji wa huduma. Toeni huduma zinazoendana na wakati,
mahitaji ya soko na kuzingatia uhitaji wa makundi mbalimbali katika jamii.
Suala hili liende sambamba na kuwaunganisha wajasiriamali na fursa mbalimbali
zinazotolewa na sekta ya fedha katika kukuza na kuimarisha biashara zao.”
Kadhalika, Mheshimiwa
Majaliwa amewataka wasimamizi wa Sekta ya Fedha na wadau wengine wazingatien
sheria na kanuni za kuwalinda watumiaji wa huduma za fedha ikiwemo kutatua
malalamiko na migogoro na kulipa fidia na mafao kwa wakati.
Amesema lengo la maadhimisho
ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa na Maonesho ya Huduma za Fedha yamejikita
katika kujenga uelewa kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya huduma za fedha
zinazotolewa, kusimamia vizuri rasilimali fedha ikiwa ni pamoja na kuimarisha
utamaduni wa kujiwekea akiba, kukopa kutoka vyanzo salama na njia sahihi za
kulipa madeni ili kujenga uchumi na kuondoa umaskini.
Naye, Waziri wa Fedha, Dkt.
Mwigulu Nchemba amesema Serikali inaendelea kukuza uelewa kwa Watanzania kuhusu
masuala ya kifedha huku akitoa wito kwa Watanzania kuweka utaratibu wa kusoma
vigezo na masharti ya huduma za kifedha wanazopata kutoka katika taasisi
mbalimbali za kifedha ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza baadae.
"Ni vyema tukaweka
utaratibu wa kusoma na kuelewa vigezo na masharti tunapokuwa tunapatiwa huduma
za kifedha hasa mikopo ili tujiepushe kuingia kwenye mikopo yenye masharti
magumu ambayo wakati mwingine tunaweza kushindwa kuyatekeleza."
Kwa Upande wake, Katibu Mkuu
wa Wizara ya Fedha Bi. Natu El-maamry amesema maadhimisho hayo ya tatu ni
muendelezo wa jitihada za Serikali katika kuongeza uelewa wa masuala fedha kwa
Watanzania ili waweze kuwa na uelewa kuhusu matumizi sahihi ya huduma za
kifedha.
Amesema taasisi mbalimbali
za kifedha na wadau wa kisekta wanatumia kipindi hiki kutoa elimu na huduma kwa
wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni