Wakala wa Usajili wa
Biashara na Leseni (BRELA), imekabidhi vifaa vya michezo truck suits jozi 25
pamoja na mipira mitano kwa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA)
vitakavyotumiwa na timu ya netiboli Wanawake, Taifa Queens.
Akikabidhi vifaa hivyo leo
tarehe 22 Novemba, 2023, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bi. Loy Mhando
amesema BRELA ni mdau mkubwa wa michezo, kwakuwa inatambua kuwa michezo ni
afya, ni burudani pia kupitia michezo Taasisi inajitangaza na zaidi ya hapo
michezo ni biashara hivyo kama Taasisi inayohusika na masuala ya urasimishaji
biashara ina wajibu wa kushirikiana na wana michezo nchini.
"BRELA imekuwa ikishiriki katika michezo
mbalimbali na kutoa misaada kwa wadau wa michezo ili kuhakikisha kuwa sekta ya
michezo nchini inakuwa na kujipambanua kimataifa", amefafanua Bi. Mhando.
Aidha Bi. Mhando amesema
msaada wa vifaa uliotolewa unaunga mkono jitihada za Mhe. Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhamasisha ukuaji wa sekta
ya michezo nchini.
Kwa upande wake Katibu Mkuu
wa CHANETA, Bi. Rose Mkisi ameishukuru BRELA kwa msaada wa vifaa vya michezo
kwa timu ya Taifa Queens.
“Tunaishukuru sana BRELA kwa
msaada wa vifaa vya michezo na tunaahidi kupitia vifaa hivi vya michezo timu ya
Netiboli itafuzu vyema katika michuano mbalimbali watakayoshiriki.
BRELA imetoa msaada wa vifaa
hivyo baada ya kupokea maombi kutoka CHANETA kuhusu uhitaji wa vifaa vya
michezo vitakavyotumika katika mashindano mpira wa pete nchini Botswana.
Hafla hiyo ya makabidhiano
ya vifaa vya michezo imefanyika katika Ofisi za BRELA jijini Dar es Salaam.
0 Maoni