Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii Mhe. Dastan Kitandula amelielekeza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania
(TANAPA) kuiunganisha Hifadhi ya Taifa Mkomazi na utalii wa Zanzibar ili
kuongeza idadi ya watalii wanaoitembelea hifadhi hiyo.
Akiwa katika ziara ya kikazi
katika hifadhi ya Taifa Mkomazi wilayani Same Mkoani Kilimanjaro, Mhe.Kitandula
alisema, "Hakuna haja ya kuachia makundi makubwa ya watalii wanaozulu
Zanzibar na kuondoka wakati mmeboresha viwanja vya ndege, hivyo ni wajibu wa
TANAPA kutumia fursa na mikakati ya kuwashawishi watalii kutoka Zanzibar kuja
kuwaona Faru na wale wanyama wakubwa 5 (The big 5)".
Aidha, Mhe.Kitandula pia ameisisitiza
hifadhi hiyo yenye sifa ya kuwa na Faru kujitanga ndani na nje ya nchi hasa
katika Bara la Asia ambalo raia wake wanasafiri katika makundi makubwa.
Alisema, "Tukibahatika kuwashawishi watalii hawa tutaongeza idadi na mapato
na kufikia adhma ya serikali kabla 2025."
Naibu Waziri huyo pia,
alilipongeza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kazi nzuri
wanayoifanya ya kuvitangaza vivutio inayopelekea kuongezeka kwa watalii, hata
hiyo aliwataka kuongeza jitihada za kukabiliana na wanyama waharibifu wakiwemo
tembo.
Afisa Mhifadhi Mkuu Kitengo
cha Utalii - Mkomazi Happiness Kiemi alimshukuru Mhe. Naibu Waziri na kuahidi
kuyafanyia kazi maagizo yote aliyoyatoa ikiwemo utatuzi wa migogoro ya
wanyamapori waharibifu.
Mhifadhi Kiemi alisema kuwa
hifadhi hiyo imeboresha miundombinu ya utalii ikiwemo ujenzi wa lango la
kuingilia wageni pamoja na viwanja vya ndege ili kurahisi safari za kuingia
hifadhini na kutoka.
Hifadhi ya Taifa Mkomazi ni
mojawapo ya hifadhi zilizoko Kaskazini mwa Tanzania ikisifika kwa kuwa na idadi
kubwa ya faru weusi na inapatikana katika mikoa ya Kilimanjaro na Tanga.
Na. Mwandishi wetu - Mkomazi
0 Maoni