Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf
Mkenda amewaomba Wamiliki wa Shule zisizo za Serikali nchini kuwekeza katika
ujenzi wa miundombinu ya mafunzo ya amali ambayo Serikali ya Awamu ya Sita
inatarajia kuyatilia mkazo kama mapendekezo ya Rasimu ya Sera ya Elimu na
Mafunzo ya Mwaka 2014 toleo la 2023 na mabadiliko ya Mtaala wa Elimu ya Awali,
Msingi, Sekondari na Ualimu yatapitishwa na Mamlaka husika.
Waziri Mkenda ameyasema hayo, 2023 jijini Dodoma wakati
akifungua Mkutano kati ya Wizara hiyo na Wamiliki wa Shule mbalimbali nchini.
Amesema kuwa, Serikali itajitahidi kwa kadri ya uwezo wake
kuona ni kwa jinsi gani watasaidia Sekta Binafsi ambao watapenda kuwekeza
katika mkondo wa mafunzo ya amali kwani Serikali pekee haitoweza kuanza kwa
kasi kwa sababu lazima kuwe na uwekezaji wa kutosha kwani ni dhahiri kuwa watu
wataunyanyapaa mkondo wa mafunzo ya amali kama utaanzishwa bila kuwekeza vya
kutosha.
“Kuna baadhi ya Shule za Mafunzo ya Amali zipo, zingine
tutazifufua, lakini tutaziongezea zaidi. Tunapenda kuwahamasisha wawekezaji
wanaohitaji kuwekeza kwenye sekta binafsi wawekeze kwenye upande wa mafunzo ya
amali, nawaomba tushikane mikono kwa pamoja kwani tunawahitaji sana kuwekeza
katika mkondo huu.” amesema Prof. Mkenda.
Vile vile, amewashukuru Wamiliki wa shule mbalimbali nchini
pamoja na wadau wa elimu kwa kuwekeza katika ujenzi bora wa shule ambapo
wameongeza fursa kwa wazazi kuchagua ni wapi wawapeleke watoto wao kupata elimu
bora hapa hapa nchini kwani zamani wengi wao walikuwa wakisafiri hadi nje ya
nchi kutafuta shule zilizo bora.
“Rais wetu Samia Suluhu Hassan kati ya vitu ambavyo
vinamtambulisha ni kuweka msukumo mkubwa na wepesi wa kufanya biashara na
kukuza uwekezaji ivyo, katika kutekeleza maelekezo ya Rais wetu tumeona
tuwasikilize ili tufahamu ni nni tunatakiwa kukifanya kuleta wepesi katika
uwekezaji na uendeshaji wa shule zetu, nyie sio maadui wala changamoto bali
ninyi ni fursa na msaada mkubwa kwa Serikali katika kuimarisha elimu.”
Akifafanua kuhusu kuanza kutumika kwa mitaala mipya ya
elimu, Waziri Mkenda amesema, mitaala hiyo inatarajiwa kuanza Januari, 2024
kwani vitabu vya ziada na kiada vilivyopo bado ni muhimu na vitatumika, kikubwa
ni kuandaa Walimu ambao nao mabadiliko ya utoaji mafunzo sio makubwa.
Amemalizia kwa kufafanua kuwa kama mapendekezo
yatakayojadiliwa katika kikao hicho yatapita kama yalivyokuwa, mitaala mipya
itaanza kutumika kwa wanaoanza Shule ya Msingi mpaka waliopo darasa la tatu
ambao watakamilisha elimu ya msingi darasa la sita lakini itakuwa ni lazima
kuendelea na shule mpaka kidato cha nne, wengine watakaoanza na mitaala hiyo ni
Kidato cha Kwanza, Kidato cha Tano na Elimu ya Ualimu mwaka wa kwanza.
Na. Jacquiline Mrisho- MAELEZO
0 Maoni