Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi
wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha
inainua ustawi wa vijana kiuchumi.
Hayo yamesemwa leo Oktoba 24, 2023 na Waziri wa Maliasili na
Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) katika Maadhimisho
ya Siku ya Umoja wa Mataifa katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
Waziri Kairuki alisema njia mbalimbali zimekuwa zikitumika
na serikali katika kuhakikisha kwamba vijana wanapiga hatua kiuchumi.
"Kwa upande wa Tanzania Bara, Sera ya Taifa ya
Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 inafanyiwa mapitio ili kuakisi hali ya sasa
ya maendeleo ya vijana, vipaumbele na changamoto," Mhe. Kairuki
amesisitiza.
Ametaja moja ya mkakati ni kuwezesha vijana kupitia Baraza
la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambalo hutoa mikopo kwa vijana
wajasiriamali na uanzishwaji wa zaidi ya mifuko 45 maalum katika wizara na
idara mbalimbali ili kuhakikisha kuwa vijana wanawezeshwa kiuchumi.
Amefafanua kuwa Serikali ya Tanzania imehakikisha kuna
ongezeko la upatikanaji wa huduma za ushauri nasaha rafiki kwa vijana kupitia
programu ya Afya ya Ujinsia na Haki za Uzazi na kuongeza upatikanaji wa huduma
za matunzo na matibabu ya VVU.
Amesema kupitia Mpango wa Kujenga Kesho Bora, YOUTH
INITIATIVE FOR AGRIBUSINESS, Serikali inatarajia kuongeza ushiriki wa vijana
katika sekta ya kilimo na kuharakisha kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo kwa
ajili ya maisha endelevu na bora.
Kufuatia juhudi hizo, bado vijana wameendelea kukumbwa na
changamoto mbalimbali hivyo, Mhe. Kairuki amezitaka jumuiya zote za Umoja wa
Afrika, Umoja wa Mataifa na Mashirika mengine ya Kikanda kuwa na nguvu ya
pamoja ili kuweka sera na mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto hizo.
Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki amewaasa vijana kuwa
wabunifu na kutumia teknolojia ambayo ni nguzo muhimu za kukuza uwezeshaji wa
vijana.
"Ni muhimu kusaidia wajasiriamali wachanga katika
kubadilisha mawazo yao kuwa biashara zinazofaa, endelevu kupitia kujenga uwezo
na upatikanaji wa masoko na matumizi ya teknolojia na uvumbuzi," amesema
Mhe. Kairuki.
Kaulimbiu ya Siku ya Umoja wa Mataifa ni: “Kuinua Idadi ya
Vijana wa Tanzania”
0 Maoni