Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry
Silaa ameelekeza watendaji wa sekta ya ardhi nchini kuhakikisha ndani ya siku
mia moja kuanzia sept 4, 2023 wanatatua migogoro ya ardhi kwa kadri ya uwezo wa
nafasi zao.
Aidha, ametaka waliovamia maeneo ya wazi kuanza kuondoka
mara moja huku akielekeza viongozi na watendaji wa wizara ya ardhi wenye
mamlaka ya kusimamia sheria kuhakikisha ndani ya siku hizo mia moja maeneo hayo
yanakuwa wazi.
Waziri Silaa ametoa kauli hiyo wakati akizumgumza na
Menejiment ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi mara baada ya
kukabidhiwa ofisi na mtangulizi wake Dkt Angeline Mabula jana katika ofisi za
wizara hiyo eneo la Mtumba Dodoma.
"Nawaomba na kuwaelekeza watendaji wote ambao sheria
imewapa mamlaka kwa kiasi chao cha kutatua migogoro ndani ya siku hizi mia moja
atatue kwa kadri ya uwezo wake,” alisema Waziri Silaa.
Waziri huyo wa Ardhi amewataka pia watendaji wa sekta ya
ardhi kusimamia haki halali wakati wa kutekeleza majukumu yao bila kujali sura wala
rangi huku akionya wanaotumia fedha kunyima haki za wengine.
Silaa alielezea pia suala la migogoro ya matumizi ya ardhi
kwenye maeneo mbalimbali na kubainisha kuwa, maelezo ya Rais Samia Suluhu
Hassan katika utatuzi wa migogoro ya à rdhi katika maeneo wanayoishi wananchi ni
lazima busara itumike.
"Mhe Rais ameelekeza katika utatuzi wa migogoro ya
ardhi katika maeneo ambayo wananchi wanaishi busara itumike, kwa sababu wale ni
watu na wakati mwingine maamuzi yakifanyika kuwaondosha athari inaweza kuwa
kubwa kuliko faida, naomba hilo mlizingatie," alisema Waziri Silaa.
Akigeukia suala la ufanisi kazini, Silaa ametaka mabadiliko
makubwa katika utendaji ili kuleta ufanisi wa kazi huku akiahidi kuwepo mifumo
mizuri itakayohakikisha kazi wanazofanya watendaji zinapimika, kuelekezeka
sambamba na kuifanya serikali ya CCM imeweza kutekeleza ahadi zake kwa
wananchi.
Kuhusu mifumo ya Tekonolojia ya Habari na Mawasiliano
(TEHAMA), amesema amesikitika kuona watu wakielezea matumizi ya mifumo huku
wananchi wakiendelea kwenda kwenye ofisi kuhitaji baadhi ya huduma za mifumo
hiyo.
"Tunafanya kazi in a primitive way, kazi very manual na
tukiendelea hivyo efficiency ya wizara itazidi kupungua na huku tunakoelekea
tutaipeleka nchi katika eneo baya, tuna kazi ya kufanya, tuwe na modern ICT
system tu na tuwe modern app ili watu waweze kuzungumza na wizara na kujiona
huru,’’ alisema Waziri Silaa.
Pia alielezea suala la vituo vya mafuta na kubainisha kuwa
ipo Kanuni ya Mwaka 2018 inayotaka kituo cha mafuta kiwe umbali wa mita za
mraba 400 yaani mita 20 kwa 20 na kuweka kuwa kuanzia tarehe 1 sept 2023 wote
walioomba kinyume na kanuni hiyo maombi yao yasimamishwe watakapokutana na
kushauriana.
Awali wakati wa makabidhiano ya ofisi aliyekuwa Waziri wa
Ardhi Dkt Angeline Mabula alisema, alipoingia na anapoicha wizara hiyo ana
imani iko kwenye hali nzuri zaidi na ni imani yake Waziri Silaa atakuwa hana
changamoto nyingi kama alivyozikuta wakati anakabidhiwa wizara.
‘’Nimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan sekta ameisogeza vizuri na tunakwenda na tukumbuke ameifungua nchi uwekezaji unakuja kwa kasi na sisi kama wizara ndiyo tunamiliki ardhi,’’ alisema Dkt Mabula.
Na Munir Shemweta, WANMM
0 Maoni