WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hadi kufikia sasa China
imewekeza zaidi ya dola bilioni 10 katika maeneo mbalimbali nchini na ametumia
fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wengine zaidi.
Majaliwa amesema kuwa takwimu za Kituo cha Uwekezaji
Tanzania (TIC) zinaonesha kuwa kuna zaidi ya miradi 1,134 ambayo imesajiliwa
kutoka makampuni ya China na hivyo kuchangia ajira kwa Watanzania.
Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo jana jioni wakati
akifunga Kongamano la Uwekezaji na Biashara baina ya Tanzania na China kwa
udhamini wa Jimbo la Zhejiang (Jinhua) kwenye hoteli ya Rotan jijini Dar es
Salaam.
“Miaka 10 iliyopita, China ilikuwa nchi ya sita miongoni wa
wawekezaji wakubwa hapa nchini ikitanguliwa na Uingereza, Marekani, Afrika
Kusini na Kenya. Lakini kutokana uwekezaji wa sasa, imekuwa nchi ya kwanza kwa
uwekezaji hapa nchini,” amesema Majaliwa.
Amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira bora na rafiki ya uwekezaji
ikiwemo kufanya maboresho ya sera ya uwekezaji. “Tumewahakikishia kuwa
tumefanya maboresho kwa kuondoa urasimu, mlolongo wa vikwazo kwa kuweka one
stop centre kwenye kituo chetu cha uwekezaji.”
Ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekeze Dodoma ambako ni
makao makuu ya nchi hasa kwenye maeneo ya ujenzi wa makazi na ofisi.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa
kongamano hilo, Waziri wa Nchi (OR- Mipango na Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo
alisema kongamano hilo limehudhuriwa na wafanyabiashara 300 wakiwemo 200 kutoka
Tanzania na 100 kutoka China.
Amesema kuandaliwa kwa kongamano hilo ni maelekezo ya Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akisisitiza suala la kuvutia wawekezaji
nchini.
Naye Balozi wa China hapa nchini, Bi. Chen Mingjian alisema
tangu kumalizika kwa ugonjwa wa UVIKO-19, uwakilishi wa makundi nane ya
wafanyabiashara kutoka miji na majimbo ya China yamekwishatembelea Tanzania ili
kuangalia fursa mbalimbali za uwekezaji.
“Kutokana na uwekezaji wa wafanyabiashara kutoka China,
bidhaa za saruji, chuma, ceramics, vifaa vya ujenzi na bidhaa za urembo na
sabuni zimezalishwa nchini na kutoa ajira zaidi ya 150,000,” alisema.
Naye Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe
alisema wafanysbiashara wa China wanakaribishwa kuwekeza katika sekta
mbalimbali hasa kwenye viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na
bidhaa nyingine zinazozalishwa nchini.
“Tunaamini tukiwa na viwanda hivyo, tutaongeza ajira kwa
vijana wetu lakini pia tutaweza kuuza nje ya nchi bidhaa zilizoboreshwa badala
ya kuuza mali ghafi.”
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni