Watoto 109,514 kupatiwa chanjo ya polio Wilayani Nkasi

 Katika utekelezaji wa zoezi la Kampeni ya chanjo ya matone dhidi ya ugonjwa wa Polio, Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa inatarajia kutoa chanjo kwa watoto 109, 514.

Hayo yamebainishwa na Mganga Mkuu wa Halmashuri ya Nkasi Dkt.Benjamin Chota ambapo amesema hamasa na elimu ilishaanza kutolewa katika maeneo mbalimbali ikiwemo kanisani, misikitini pamoja na redio jamii Nkasi Fm.

“Sisi kama Halmashauri tulianza kutoa hamasa na elimu katika maeneo mbalimbali na lengo ni kuwafikia watoto 109,514 wenye umri chini ya miaka 8 na sehemu kubwa ambayo tunategemea kuwapata watoto ni maeneo ya shuleni na nyumba kwa nyumba pia,” alisema Dkt. Chota.

Aidha, Dkt. Chota ametoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha zoezi la kampeni ya Polio kwani mtoto asipopata chanjo anaweza kupata ulemavu wa kudumu.

 “Ni chanjo muhimu kuwakinga watoto wetu na ugonjwa wa kupooza na madhara makubwa ni ulemavu wa kudumu hivyo, jamii naiomba kutoa ushirikiano pindi timu za uchanjaji zinapopita ikiwezekana tupate watoto wengi zaidi ya lengo” alisema Dkt. Chota.

Ikumbukwe kuwa Kampeni ya Chanjo ya Matone dhidi ya ugonjwa wa Polio inatarajiwa kuzinduliwa tarehe 21, Septemba 2023 katika Viwanja vya Ndua Wilayani Sumbawanga Mkoani Kagera na Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu na itafanyika hadi Septemba 24, 2023 katika mikoa 6 ya Rukwa, Kagera, Kigoma, Katavi, Songwe na Mbeya huku walengwa ni watoto wote walio chini ya miaka 8.

Chapisha Maoni

0 Maoni