Wapiga kura 216,282 walioandikishwa kwenye Daftari la Kudumu
la Wapiga Kura wanatarajiwa kupiga kura kesho tarehe 19 Septemba, 2023 kwenye
uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mbarali na kata sita za Tanzania Bara.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa
Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele ameyasema hayo Wilayani Mbarali, Mkoani
Mbeya leo tarehe 18 Septemba, 2023 wakati akisoma risala kwa ajili ya uchaguzi
huo na kuongeza kwamba uchaguzi utahusisha vituo 580 vya kupigia kura.
“Katika uchaguzi huu kuna jumla ya wapiga kura 216,282
walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambao watashiriki
kuchagua viongozi wao. Aidha, uchaguzi
huu utahusisha vituo 580 vya kupigia kura vilivyobainishwa,” amesema Jaji Mwambegele.
Kata zenye uchaguzi ni; Nala iliyopo Halmashauri ya Jiji la
Dodoma, Mfaranyaki iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Mwaniko iliyopo
Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Old Moshi Magharibi iliyopo Halmashauri ya
Wilaya ya Moshi, Marangu Kitowo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rombo na
Mtyangimbole iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.
Mwenyekiti wa Tume amevikumbusha vyama vya siasa, wagombea,
mawakala wa vyama, wapiga kura na wananchi kwa ujumla kuhakikisha kwamba
hawapigi kampeni siku ya kupiga kura kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha
sheria.
“Alama za vyama vya siasa zinazoashiria kampeni kama vile
vipeperushi, bendera na mavazi haviruhusiwi kutumika kesho tarehe 19 Septemba,
2023 ambayo ni siku ya uchaguzi,” amesema.
Jaji Mwambegele ameongeza kwamba zoezi la kupiga kura katika
maeneo yote ya uchaguzi litafanyika katika vituo vile vile vilivyotumika wakati
wa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.
Ameongeza kwamba vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa
moja kamili (1:00) asubuhi na kufungwa saa kumi kamili (10:00) jioni.
“Iwapo, wakati wa kufunga kituo watakuwepo wapiga kura
katika mstari ambao wamefika kabla ya saa kumi kamili (10:00) jioni katika
mstari na hawajapiga kura, wataruhusiwa kupiga kura. Mtu yeyote hataruhusiwa
kujiunga katika mstari wa wapiga kura baada ya saa kumi kamili (10:00) jioni,”
amesema.
Jaji Mwambengele amebainisha kwamba watakaoruhusiwa kupiga
kura ni wale tu ambao wamo kwenye
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye kata husika na wana kadi zao za
mpiga kura.
Ameongeza kuwa, hata hivyo, Tume kwa kuzingatia masharti ya
kifungu cha 61(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 pamoja na
kifungu cha 62(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292
imeruhusu wapiga kura ambao wamepoteza kadi zao au kadi kuharibika kutumia
vitambulisho mbadala.
“Mojawapo ya kitambulisho mbadala ambacho mpiga kura anaweza
kutumia ni Pasi ya Kusafiria, Leseni ya Udereva au Kitambulisho cha Taifa
kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA),” amesema.
Mwenyeki wa Tume amesisitiza kwamba ili mpiga kura aruhusiwe
kutumia kitambulisho mbadala ni sharti awe ameandikishwa kwenye Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura na jina lake lipo katika orodha ya wapiga kura katika
kituo anachokwenda kupiga kura.
“Katika kituo cha kupigia kura, kipaumbele kitatolewa kwa
wagonjwa, watu wenye ulemavu, wazee, wajawazito na akina mama wanaonyonyesha
watakaokwenda na watoto kituoni,” amesema.
Kuhusu wapiga kura kurudi nyumbani baada ya kupiga kura,
Jaji Mwambegele amesema hilo ni sharti la kisheria na kwamba maadili ya
uchaguzi yaliyosainiwa na kuridhiwa na vyama vyote vya siasa, Serikali na Tume
yanaelekeza hivyo.
Alisisitiza kwa kusema “wapiga kura watatakiwa kuondoka
kituoni mara wanapomaliza kupiga kura ili kuepusha msongamano na vitendo
vinavyoweza kuchochea uvunjifu wa amani.
Hivyo, Tume inawashauri wananchi kujiepusha na mikusanyiko katika maeneo
ya vituo vya kupigia kura”.
Ametoa rai kwa wapiga kura katika Jimbo la Mbarali na kata
sita zinazohusika na uchaguzi huu mdogo, kujitokeza kwa wingi kwenye vituo vya
kupigia kura, ili kuwachagua viongozi wanaowataka.
Jumla ya vyama 17 vya siasa vinashiriki kwenye uchaguzi huo
mdogo, vyama hivyo vinajumuisha AAFP, ACT–WAZALENDO, ADA–TADEA, ADC, CCK, CCM,
CUF, Demokrasia Makini, DP, NLD, NRA, SAU, TLP, UDP, UMD, UPDP na NCCR–MAGEUZI.
Mwisho.
0 Maoni