Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza limewaonya watu wanaofanya uhalifu
kwenye Ziwa Victoria pamoja na wanaojihusisha na uvuvi haramu na kusema hatua
kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa
ametoa kauli hiyo wakati akitoa elimu ya kuzuia uhalifu kwa wananchi wa Kata za
Bugogwa, Sangabuye, Shibula na Kayenze Wilayani Ilemela ikiwa ni muendelezo wa
ziara yake iliyolenga kutoa elimu ya kuzuia uhalifu kwa wananchi wa mkoa huo.
Kupitia kikao hicho Kamanda Mutafungwa akatangaza msako kwa
wahalifu wanaopora vyavu za wavuvi na mazao ya uvuvi huku akiahidi kuwachukulia
hatua za kisheria watakaobainika.
"Kuanzia leo msako mkali wa kuwasaka wahalifu katika
maeneo yote unaendelea, watafute pa kwenda maana inakuja oparesheni kali ambayo
itawapa wakati mgumu sana wahalifu tunachoomba kutoka kwenu wananchi ni
ushirikiano maana mpaka sasa tuna majina ya wahalifu na tutawafuata popote
walipo iwe majini au nchi kavu," amesema Kamanda Mutafungwa.
Katika hatua nyingine Kamanda Mutafungwa amekemea vitendo
vya imani za kishirikina ikiwemo Kamchape na Lambalamba na kuwataka
wanaoendesha shughuli hizo kujisalimisha wenyewe kwa Jeshi la Polisi kabla
hawajaanza kusakwa.
0 Maoni