Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, amesema kuwa
ifikapo mwezi Desemba mwaka huu, utekelezaji wa Mradi wa Kusambaza Umeme
Vijijini wa Awamu ya Tatu mzunguko wa Pili katika vijiji vyote utakamilika, hivyo kupelekea kuanza utekelezaji wa mradi wa kupeleka umeme vitongojini.
Kapinga amesema hayo wakati wa ziara yake ya kukagua
maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo katika Mkoa wa Tabora ambapo katika siku
ya pili ya ziara yake amewasha umeme katika kijiji cha Katunda wilayani Uyui
mkoani humo.
“Tunatarajia kumaliza kazi ya kusambaza umeme vijijini
ifikapo mwezi Desemba mwaka huu, nawahimiza wakandarasi fanyeni kazi yenu kwa
uadilifu mkubwa, hatuhitaji kukimbizana juu ya hilo kila mmoja atekeleze jukumu
lake kwa maslahi mapana ya taifa letu”, alisema Kapinga.
Kapinga amewaagiza wakandarasi wote nchini kuhakikisha kuwa
vifaa vya kufanyia kazi vinakuwepo wakati wote katika maeneo ya miradi ili
kurahisisha utekelezaji wa mradi huo na hivyo kuukamilisha kwa wakati.
Pia, amewataka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kukagua
vifaa vya wakandarasi ili kujihakikishia kama vipo vyote katika karakana zao
ili kuhakikisha kuwa kazi zinafanyika kwa wakati na zinaendana na muda wa
mkataba uliowekwa.
Vilevile, amewataka REA kuchukua hatua stahiki kwa
wakandarasi wote watakaokwenda kinyume na makubaliano ya mikataba ya kupeleka
umeme vijijini.
Kapinga amewaagiza REA kuendelea kuwasimamia wakandarasi kwa
karibu kwakuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha fedha inazozitoa zinaenda
kuwafikishia wananchi umeme kama alivyoelekeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Naibu Waziri wa Nishati amewasisitiza wananchi kuendelea
kusuka nyaya katika nyumba zao ili kujiweka tayari kuunganishiwa umeme pindi
utakapowafikia katika maeneo yao na kwamba watu wote watafikiwa na umeme.
Pia alizungunza na wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO) mkoani Tabora na kuwaeleza kuwa watanzania wanataka umeme hivyo
wafanye kazi kwa weledi, juhudi na maarifa usiku na mchana kuhakikisha
watanzania wote wanapata umeme na kuwatatulia changamoto za umeme
zinazowakabili wananchi hao.
Na. Zuena Msuya, na Theresia Lugwisha- Tabora
0 Maoni