Imeelezwa kwamba ukatili wa urembo kwa watoto ni tatizo
linalochukua sura mpya kwenye jamii ukiambatana na madhara ya kiafya, kijamii
na kisaikolojia.
Hayo yamebainika Septemba 26, 2023 jijini Dar es Salaam
wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Sauti ya Watoto Tanzania (SAWATA) yenye lengo
la kuelimisha jamii kuhusu kulinda watoto dhidi ya ukatili huo na kutoa maoni
juu ya mikakati ya kisera kwa ajili kudhibiti ukatili huo.
Akizungumza na wanahabari Mwenyekiti wa SAWATA Jessica Juma
amesema lengo la Taasisi hiyo iliyoanzishwa baadhi ya wananchi ni kupambana na
ukatili kwa watoto dhidi ya urembo ili kulinda ustawi na ulinzi wa haki za
mtoto iliyo na kaulimbiu isemayo Sauti Yetu, Watoto Wetu.
"Tumejitolea kuungana na Serikali kupaza sauti kwenye
jamii katika nyaja ya urembo wenye madhara kwa watoto kwani kumekuwa na ukatili
unaoendelea kuwahusu watoto katika nyanja ya urembo," amesema Jessica.
Kwa upande wake Daktari Gasper Shayo kutoka Hospitali ya
Rufaa ya Mwananyamala ametoa wito kwa jamii kuacha kuwalazimisha watoto
kufanyiwa urembo hasa unaohusisha kemikali kwani una madhara kwa watoto.
"Kampeni hii
itatusaidia pia madaktari kuwaelimisha wananchi, kwani tumekuwa tukipokea
wagonjwa mara kadhaa watoto wakiwa wameathirika na bidhaa za urembo zenye
kemikali," amesisitiza Dkt. Shayo.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi
Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizindua Kampeni hiyo, amesema urembo na
mapambo hasa ya kemikali yanaweza kuwa na athari mbaya kwa watoto, kiafya,
kijamii na kisaikolojia hivyo wazazi na walezi wazingatie hilo ili kumlinda
mtoto na athari hizo.
Ameipongeza Taasisi ya SAWATA na kuahidi Wizara itaendelea
kushirikiana nao pamoja na wananchi wote wenye ajenda kama hizo kuisadia jamii
kuondoka na changamoto mbalimbali zilizopo.
Waziri Dkt. Gwajima amesisitiza kwamba athari za ukatili wa
urembo ni pamoja na watoto kutojiamini kuhusu muonekano wao, maambukizi ya
ngozi, watoto kujitenga wanapokosa urembo na kushindwa kutambua tofauti ya
urembo halisi na ule wa mapambo.
"Kwa kuzingatia athari hizo ni dhahiri kuwa kampeni hii
ni muhimu sana katika kuhakikisha watoto wa Tanzania wanakua na kujenga maisha
yao bila kudhurika kisaikolojia au kimwili kutokana na masuala ya urembo,"
amesisitiza Waziri Dkt. Gwajima.
Na WMJJWM- Dar es Salaam
0 Maoni