Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa
amewataka watumishi wa Wizara yake kuhakikisha wanawahudumia vizuri wananchi
ili wajenge imani na serikali.
‘’Lazima tutengeneze ‘despline’ ya wizara kwa kuwahudumia
vizuri wananchi, tukumbuke hapa tunafanya kazi ya watanzania kwa niaba ya Rais
Samia Suluhu Hassan,’’ alisema Waziri Silaa.
Akizungumza na watumishi wa Wizara ya Ardhi baada ya
uzinduzi wa Kituo cha Taifa cha Ubunifu na Mafunzo ya Taarifa za Kijiografia,
Waziri Silaa amesema, wakati wa kutekeleza majukumu, watumishi hao wakumbuke
kuwa siyo kila mwananchi ana haki lakini wanao wajibu wa kutenda haki wakati
wote wa utekelezaji majukumu.
‘’Mna wajibu wa kusimamia haki na kila mtu atolee maamuzi
kwa kazi inayowasilishwa kwake na kama mwananchi hapaswi kupewa kiwanja aelezwe
bayana kwa maandishi,’’ alisema Mhe. Silaa.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi, wizara yake kwa sasa
inakwenda kufanya maboresho yanayolenga kuleta tija ambapo amewataka watumishi
wa sekta ya ardhi kuwa tayari kwa maboresho hayo.
‘’Mtu anafuatilia hati kwa zaidi ya miezi mitatu hapo kuna
‘question mark’ hata kama ni urasimu utakuwa umepitiliza,’’ alisema Mhe. Silaa.
Amewaeleza waumishi wa Wizara hiyo kuwa, pamoja na kuelezwa
mambo mengi ya wizara yake lakini ana haki ya kusikiliza na kubainisha kuwa,
atazitumia siku mia moja kujifunza ili watakapokutana kwenye maeneo ya kazi
ajue cha kufanya.
Kikao hicho cha Waziri Silaa na watumishi kimehusisha
viongozi wa Wizara, baadhi ya watumishi kutoka Makao Makuu, Ofisi za Ardhi za
Mikoa pamoja na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi.
Na Munir Shemweta, WANMM
0 Maoni