Wizara ya Afya imewasisitiza wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe kujitokeza katika zoezi la utolewaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio linalotarajiwa kuanzia tarehe 21-24 Septemba 2023 ili watoto wao waweze kupata chanjo ya ugonjwa huo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati
akiongea na madaktari, wauguzi pamoja na timu ya usimamizi wa afya ngazi ya
Halmashauri wakati alipofanya ziara katika Mkoa wa Songwe.
“Baada ya kupatikana kwa mgonjwa mmoja mwenye ugonjwa wa
Polio Mkoani Rukwa Serikali kupitia Wizara ya Afya tumeamua kutoa chanjo hiyo
kwa Mikoa Sita ikiwemo Mkoa wa Rukwa, Kagera, Kigoma, Mbeya, Katavi, Songwe
hivyo ninawaomba sana wazazi kushiriki kwa kuwatoa watoto,” amesema Waziri
Ummy.
Pia, Waziri Ummy ameiagiza Bohari Kuu ya Dawa Nchini
kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba katika Halmashauri hiyo ili Hospitali ya
Wilaya ya Songwe ianze kutoa huduma katika sehemu ambazo hazijaanza.
“MSD hakikisheni vifaa tiba vinapatikana kwa wakati na
mvigawe katika vituo vya Afya ikiwemo Hospitali ya Wilaya ya Songwe ili huduma
zipatikane ikiwemo huduma za uzazi mama na mtoto,” amesema Waziri Ummy.
Aidha, amesema Halmashauri ya Wilaya ya Songwe watapatiwa
magari matatu ya kubebea wagonjwa (Ambulance) ili kusaidia kutoa huduma za
dharura na rufaa za matibabu na kupunguza madhara makubwa yanayoweza sababisha
vifo kwa wagonjwa wanaohitaji huduma kwa haraka.
Waziri Ummy amesema Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan imeagiza kila Halmashauri kupata magari ya kubebea wagonjwa mawili na
Wizara ya Afya inatoa gari moja, jumla Halmashuri hiyo itapata magari matatu.
"Magari haya yatasaidia kupunguza vifo vya mama na
mtoto, lakini pia kurahisisha mgonjwa kupata huduma kwa haraka pale anapopatiwa
rufaa au anapohitaji huduma za dharura," amesema Waziri Ummy.
Katika ziara hiyo Waziri Ummy ameridhishwa na upatikanaji wa
dawa, utolewaji wa huduma pamoja na ujenzi unaoendelea ikiwemo jengo la EMD,
Mama na Mtoto, Utawala, Mochwari na jengo la huduma za Mionzi.
“Kwakweli nimeridhishwa na upatikanaji wa Dawa, kwa sasa
hatuwezi kumlaumu Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatoa fedha za dawa kwa
100%, Sasa kazi kwetu watendaji tuendelee kuhakikisha Dawa zinapatikana, “amesema
Waziri Ummy.
Na. WAF - Songwe
0 Maoni