Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan
Abbasi, amesema mafanikio ya filamu ya “Tanzania; The Royal Tour” ambayo Rais
Samia Suluhu Hassan alishiriki ili kuitangaza Tanzania yameendelea kuleta
mafuriko ya mafanikio katika sekta hiyo.
“Tayari kwa takwimu za Benki Kuu ya Tanzania za Julai, 2022
hadi Julai, 2023 idadi ya watalii kutoka nje imefikia milioni 1.66 na mapato
yamapaa hadi Dola za Marekani Bilioni 2.995 rekodi zote hizi hazijawahi
kufikiwa wakati wowote katika historia ya nchi hii,” alisema Dkt. Abbasi
akihutubia leo Septemba 8, 2023, kwenye mahafali ya 58 ya Chuo cha Taaluma ya
Wanyamapori Pasiansi jijini Mwanza ambacho hufundisha askari wa wanyamapori na
wataalamu wa kuongoza watalii.
Aliongeza kuwa uhifadhi ambao umechangiwa pia na wataalamu
walioandaliwa na chuo hicho kwa miaka mingi nao umelipa ambapo leo Tanzania ina
rekodi mbalimbali za Afrika na dunia ikiwemo kuwa miongoni mwa nchi za Afrika
zenye tembo na faru wengi huku ikiongoza duniani kwa kuwa na simba na chui
wengi.
Ametumia fursa hiyo kuwaomba wadau wa utalii na uhifadhi
nchini kuwaajiri na kuwatumia vijana walioandaliwa vyema ikiwemo kutoka taasisi
ya Pasiansi ili kuhakikisha utolewaji wa huduma bora katika sekta hiyo yenye
ushindani mkubwa baina ya mataifa mbalimbali.
0 Maoni