RC Makalla aweka mkakati wa kuufanya uwanja wa ndege Mwanza kuwa wa Kimataifa

 

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla, amesema Serikali ina mkakakati wa kuufanya uwanja wa Ndege wa Mwanza kuwa wa Kimataifa kwa kujenga miundombinu ya kisasa likiwemo jengo la abiria, hotel na shopping mall ili kuleta unadhifu kwenye utoaji huduma.

Makalla amesema hayo wakati akizungumza na watumishi wa uwanja huo na kusema zaidi ya shilingi bilioni 11 zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa miundombinu katika uwanja huo na kuiagiza mamlaka ya uwanja huo kuandaa michoro ya miundombinu hiyo.

"Nilikuja hapa nikiwa na siku tatu tu Mwanza na nlielekeza muanze ujenzi mara moja tena kwa bahati mna fedha za kuanzia tena ni shilingi bilioni 11 na kazi ya kwanza mliyotakiwa kuanza nayo ni kusanifu namna bora ya ujenzi wa Jengo ambalo litakua la kimataifa kwa ili ya kuubadirisha uwanja wetu kuwa wa kimataifa," amesema Makalla.

Makalla amesema shughuli za mamlaka ya viwanja vya ndege pamoja na jeshi la anga kwenye eneo hilo hazipaswi kuingiliwa na wananchi waliovamia na kwamba wameandaa utaratibu wa kuwaondoa wananchi zaidi ya elfu moja (nyumba 800) wa Mitaa ya Mhonze, Kihili na Bukyanhulu waliovamia eneo la Mamlaka ya Uwanja wa ndege ili kutoa fursa kwa shughuli za uwanja kufanyika katika hali ya usalama.

"Kwakuwa Mwanza tunaanza safari ya kuubadilisha uwanja wa ndege kuwa uwanja wa Kimataifa, Mamlaka inahitaji eneo lote na kwa ajili ya usalama pia maana jeshi la anga wanalihitaji eneo hilo pia kwa usalama wa ndege zao, za abiria na kwa usalama wa wananchi wetu pia,” amesema Makalla.

Kwa upande wake Meneja wa Uwanja wa Ndege Mwanza, Mussa Mcholla, amesema katika kuweka mazingira bora ya usafiri wa anga nchini serikali imefanya maboresho ya kimkakati yaliyohusisha urefushaji wa barabara ya kutua na kuruka ndege, ujenzi wa jengo jipya la abiria na miundombinu mingine.

"Serikali imefanya maboresho ya kimkakati kama urefushaji wa wa barabara ya kutua na kupaa, upanuzi na ujenzi wa tabaka la mwisho la lami pamoja na ujenzi wa Jango jipya la mizigo na barabara za maungio ya ndani kwa ajili ya magari na mfumo wa maji taka.


Chapisha Maoni

0 Maoni