Polisi waunga mkono juhudi za Rais Samia kutangaza utalii

 

Jeshi la Polisi limetembelea Hifadhi ya Taifa ya Arusha lengo likiwa ni kujionea vivutio vinavyopatikana katika hifadhi hiyo ambayo inapatikana ndani ya mkoa wa Arusha sambamba na kuhamasisha watu kutembelea vivutio hivyo.

Akiongoza zoezi hilo kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi hilo, CP Awadh Haji alisema wameona fahari kutembelea hifadhi hiyo yenye vivutio mbalimbali ikiwa ni kuunga juhudi za Mheshimiwa Rais za kuutangaza utalii wa Nchi yetu.

CP Awadh alibainisha kuwa ziara hiyo itachangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha uhusiano, kutatua changamoto za kiusalama baina ya Jeshi hilo na wadau wengine wanaohusika moja kwa moja kuhudumia watalii.

Sambamba na hilo pia alisema Jeshi hilo limeingia mkataba wa mashirikiano na Chuo cha Taifa cha Utalii ili kuwajengea uwezo wa kiutendaji Maafisa, Wakaguzi na Askari ili kuhakikisha wanakwenda kutoa huduma bora kwa watalii na wageni wote wanaofika nchini.

‘’Dhamira ya Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu ni kukuza Utalii wa nchi yetu na kuongezeka idadi ya watalii nchini, hivyo sisi Jeshi la Polisi tutahakikisha tunaenda kutoa huduma bora kwa watalii na wageni wanaofika nchini sambamba na kuimarisha usalama wao,” alisisitiza CP Awadh.

Kwa upande wake Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo ACC Yustina Kiwango alisema wamekua na mahusiano mazuri na jeshi la Polisi ambapo mara nyingi hufanya operesheni za pamoja hali ambayo inapelekea Watalii wanaotembelea hifadhi hiyo kufurahia mandhari bila ya uwepo wa changamoto za kiusalama.

Aidha, ametoa wito kwa taasisi nyingine za serikali na za binafsi kutembelea hifadhi hiyo ili kujionea vivutio vilivyopo sambamba na kuutangaza utalii wa Nchi yetu.

Ziara hiyo imekuja mara baada ya Jeshi hilo kuingia mkataba wa mashirikiano na Chuo cha Taifa cha Utalii jana Jijini Arusha ambapo maafisa wa Jeshi hilo watajengewa uwezo wa kiutendaji wa namna bora ya kuwahudumia watalii.

Na. Mwandishi wa Jeshi la Polisi


Chapisha Maoni

0 Maoni