WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa kituo cha
afya cha Kakunyu kilichopo kilomita 75 kutoka tarafa ya Bunazi, wilayani
Missenyi na kutoa siku tano kiwe kimeanza kufanya kazi.
Majaliwa ametoa agizo hilo jana mara bada ya kukagua kituo
hicho, wakati akizungumza na wananchi waliojitokeza kumpokea katika kijiji cha
Bugango, wilayani Missenyi, mkoani Kagera.
"Mkurugenzi, hawa madaktari wameletwa kufanya kazi.
Watafutie meza, dawa zipo, wape makaratasi yao waanze kuhudumia wananchi.
Nakupa siku tano, hapo mapokezi na vyumba vya madaktari vianze kazi sababu hawa
tayari wapo hapa kijijini," amesema Majaliwa wakati akimpa maelekezo
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, Bw. John Wanga.
Waziri Mkuu alikagua majengo yaliyokamilika ambayo ni jengo
la wagonjwa wa nje (OPD), maabara, wodi ya wazazi na kliniki ya uzazi na mtoto
(RCH). Kituo hicho kimegharimu sh. milioni 613 ambapo sh. milioni 523 ni za
mapato ya ndani na sh. milioni 90 zilitoka Serikali kuu ambazo zimetumika
kujenga nyumba moja ya kuishi watumishi watatu (3 in 1).
Waziri Mkuu aliwaeleza wananchi hao kwamba sh. milioni 150
zimekwishatolewa na Serikali ya awamu ya sita ili zitumike kununua vifaa tiba
vya kituo chao. Alipoulizwa kuhusu uwepo wa fedha hizo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa
Kagera, Dkt. Isesanda Kaniki alikiri kuwa fedha hizo zimeshapokelewa na
zimetumwa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ili kulipia vifaa tiba hivyo.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu Majaliwa amewataka wakazi hao
wachangamkie fursa za kilimo cha mazao ya chakula na biashara kwa sababu kilimo
ni fursa, kilimo ni uchumi na kilimo ni maisha.
“Endeleeni kulima mazao ya miezi mitatu mitatu kama maharage
na mahindi, ili muweze kuuza nchi za jirani. Mheshimiwa Rais alitoa sh. bilioni
50 za ruzuku ya pembejeo hasa mbolea ili mpate mbolea hiyo na kuzalisha zaidi
mazao. Jiandikisheni ili mpate namba za kudumu za kielektroniki za utambulisho.
Namba hizi zitawasaidia kupata unafuu wakati wa kununua pembejeo,” alisema.
Aidha, aliwataka wakazi hao watunze vyanzo vya maji dhidi ya
mifugo na ukataji miti hovyo kwani uharibifu wa vyanzo vya maji ni mkubwa.
“Uharibifu ni mkubwa na mifugo mingi ilikuwa inaingia kuja kuharibu vyanzo na
sisi wenyewe hatuvilindi. Serikali zote za vijiji na Kamati za Mazingira nenda
muwe wakali dhidi ya watu wanaoharibu vyanzo vyetu ili tupate maji mengi kwa
ajili ya matumizi ya vijijini, majumbani na mashambani.”
“Wenyeviti wa vijiji na kamati zenu za maendeleo za kata,
simamieni eneo la mazingira kwani hali si nzuri. Duniani leo, kuna mabadiliko
makubwa ya hali ya hewa, hata majira ya mvua yamebadilika. Kwa nini? Ni kwa
sababu tumeharibu vyanzo. Nani ameharibu? Ni sisi wenyewe. Nani atavilinda? Ni
sisi wenyewe. Hebu tuvilinde vyanzo vyetu,” alisisitiza.
Waziri Mkuu yuko mkoani Kagera kwa ziara ya siku tatu na leo
atazuru wilaya ya Muleba.
0 Maoni