Mauzo ghafi ya bima yaongezeka nchini na kufikia Sh. Trilioni 1.2

 

Sekta ya Bima nchini imekua kwa wastani wa asilimia 12.8% kwa mwaka, ambapo kwa kipindi cha miaka mitano mauzo ghafi ya bima yameongezeka kutoka shilingi bilioni 691.9 mwaka 2018 hadi kufikia takribani shilingi trilion 1.2 mwaka 2022.

Hayo yameelezwa leo na Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Baghayo Saqware wakati akitoa taarifa ya TIRA katika semina na wahariri wa vyombo vya habari nchini iliyofanyika Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Saqware amesema pamoja na mafanikio hayo TIRA imepanga kutoa elimu ya bima ili kuwafikia asilimia 80 ya Watanzania na kuongeza idadi ya watumiaji wa bima kufikia asilimia 50 kutoka idadi ya asilimia 18 ya watumiaji wa bima iliyopo sasa.

“Tunampango wa kutoa elimu ya bima kwa asilimia 80 ya Watanzania wa umri wa kuanzia miaka 18, na kuongeza watumiaji wa huduma za bima hadi kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030, kulingana na malengo yaliyowekwa na Serikali,” alisema Dkt. Saqware.

Amesema mchango wa sekta ya bima kwenye pato la Taifa unazidi kuongezeka kutoka asilimia 0.56% kwa mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 1.68% kwa mwaka 2021. Pia Mamlaka imeendelea kuongeza gawio la Serikali ambapo kwa kipindi cha Julai 2022, hadi Juni 2023 Mamlaka imeweza kulipa gawio kwa Serikali la jumla ya shilingi bilioni 2.9.

Kuhusu mchango wa sekta ya bima katika kuzalisha ajira Dkt. Saqware amesema sekta ya bima imechangia kwenye ajira kwa vijana ambapo hadi Septemba 2022 imetoa ajira za kudumu kwa Watanzania 4, 173.

Aidha, amesema mamlaka inaendelea na utekelezaji wa mkakati wa utoaji Elimu na Uhamasishaji kwa Wizara na Taasisi za Umma kutekeleza Sheria ya Bima sura Na. 394 ya 2009, na Sheria ya Manunuzi, Na.7 ya 2011.

 Amesema lengo la mkakati ni utoaji elimu ya bima na uhamasishaji wa Serikali, Idara, Taasisi za Umma ili ziweze kuzingatia Sheria ya Bima Sura 394, kif.133 (1) hadi (3), kif.140 na Sheria ya Umma Na. 7 ya Mwaka 2011, kif. 4 (2) (b).

“Hadi mwezi Julai 2023, Mamlaka imezitembelea Wizara za Kilimo, Wizara ya Nishati na Wizara ya Uchukuzi na Ujenzi na TAMISEMI na mkakati huu ni endelevu na utazifikia Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali za Umma,” amesema Dkt. Saqware.

Kuhusu ulipaji wa madai ya malipo ya bima, Dkt. Saqware amesema kwamba asilimia 95 ya madai ya malipo ya bima yanalipwa vizuri, na kuongeza kwamba ni asilimia 5 tu ya madai huwa ndio yenye changamoto ya malipo kutokana na kukosa ushirikiano wa wadai ama nyaraka sahihi zinazohitajika.

Pamoja na mambo mengine Dkt. Saqware ameeleza kuwa bima ya afya ndio inayoongoza kwa gharama za malipo ya fidia, hali inayochangiwa na ukweli kwamba gharama za matibabu ni kubwa, na pia baadhi ya watoa huduma wasiowaaminifu huongeza madai ili yawe makubwa.

Kuhusu mchango wa bima kwa soko la fedha nchi, Dkt. Saqware amesema benki nchini zinategemea sana hifadhi ya fedha za bima katika kuendeleza soko la fedha nchini.

Chapisha Maoni

0 Maoni