Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewaagiza Maafisa Utumishi wa
Halmashauri zote nchini kuacha tabia ya kukaa ofisini badala yake watembelee
ofisi za Watumishi zilizopo katika Kata na Vijiji ili kutatua changamoto za
watumishi walioko huko.
Aidha, Mhe. Kikwete amepiga marufuku tabia ya baadhi ya
Maafisa Utumishi kutoa vibali vya kusafiri kwa Watumishi kwenda Jijini Dodoma
katika Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa ajili ya kufuatilia
masuala yao binafsi ya kiutumishi ilhali kazi hiyo ni ya Maafisa Utumishi hao.
Amesema Watumishi hao hufika Dodoma kwa ajili ya kufuatilia
kupandishwa madaraja, kubadilishiwa miundo na kada, kudai malimbikizo ya
mshahara, kuwa vitendo hivyo vinawanyima fursa wananchi kuhudumiwa na Watumishi
hao waliolazimika kusafiri.
Mhe. Kikwete ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na
Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, ikiwa ni siku yake ya tatu ya
ziara anayoendelea kufanya mkoani Mara ambapo amewataka Maafisa Utumishi hao
kuleta matumaini kwa Watumishi wenzao
"Acheni ile tabia ya kuonekana miungu watu, tatueni
matatizo ya watumishi," amesisitiza Mhe.Kikwete.
Amesema Maafisa Utumishi katika Halmashauri hizo ni lazima
watambue wateja wao namba moja ni Watumishi wenzao, hivyo ni lazima wawape
kipaumbele katika kutatua changamoto zao ili kupata matokeo makubwa.
"Katika ziara zenu mtakazojipangia za kutembelea vituo
vya kazi hakikisheni mnatatua changamoto za watumishi wenu huku mkitumia nafasi
hizo kwa kuwapatia taarifa za fursa mbalimbali za kiuchumi na za kujiendeleza
kielimu zinazopatikana kwa sasa " amesema Mhe.Kikwete.
Amesema haipendezi kuona hata masuala madogo tu ya
kiutumishi yanayowakabili Watumishi wao yanasubiri hadi siku Waziri au Naibu
Waziri atoke Dodoma ndo aje kuyatatua.
Amewaeleza Maafisa Utumishi hao ni lazima wahakikishe
utendaji kazi zao unakuwa wa kimkakati na sio kufanya kazi kwa mazoea
Amesema moja ya jukumu la msingi kwa Maafisa Utumishi ni
kuhakikisha Watumishi wanaowaongoza wanatatuliwa changamoto zinazowakabili hata
ikibidi kufika Dodoma wasisite kwenda.
"Maafisa Utumishi hakikisheni mnajipangia ratiba ya
kutembelea vituo vyenu zungumzeni na kusikiliza kero za watumishi, sitegemei
nikija tena nisikie changamoto ndogo ndogo kutoka kwa watumishi wenu,
"amesisitiza Mhe. Kikwete.
0 Maoni