Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewaeleza watanzania kuwa changamoto ya kukosekana umeme wa uhakika ni ya muda mfupi kwa sababu Ujenzi wa Mradi wa Kuzalisha umeme wa JNHPP wa Megawati 2,115 umefikia asilimia 91.72 hadi sasa.
Dkt.Biteko amesema hayo wakati wa ziara yake ya kwanza
kutembelea mradi huo, tangu ateuliwe kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, iliyofanyika tarehe 16 Septemba, 2023 mkoani Pwani kwa lengo la kuona
maendeleo ya ujenzi wa mradi huo.
Amesema kuwa ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo
mkubwa na wa kielelezo kwa nchi yetu, ambapo Serikali imewekeza fedha nyingi
takribani Shilingi trilioni 6.558 ili kuhakikisha watanzania wanapata umeme wa
kutosha na wa uhakika wakati wote.
“Tupo katika hatua za mwisho za ujenzi wa mradi huu ili
tuweze kuwapatia watanzania umeme wa uhakika, waweze kukuza uchumi wao, uwepo
wa mradi huu tunaamini kwamba changamoto ya umeme tuliyonayo kwa sasa ni ya
muda mfupi kwa kuwa ujenzi wa mradi umefikia asilimia 91.72,” amesema Dkt.
Biteko.
Alifafanua kuwa tayari Serikali imekwishamlipa mkandrasi
asilimia 85.5 ya malipo yake ya kazi aliyoifanya katika hatua ya ujenzi
iliyofikiwa hadi sasa katika mradi huo.
Amemshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa msukumo mkubwa aliouweka katika kutekeleza
mradi huo.
Pia amewapongeza wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa mradi
huo, Mshauri wa mradi na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambaye ndiye
msimamizi mkuu wa mradi huo kwa niaba ya Serikali, kwa hatua kubwa iliyofikiwa.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,
Mhe. Dkt. Biteko aliambatana na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi
Felchesmi Mramba, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka,
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Maharage Chande na
viongozi wengine kutoka wizarani na TANESCO.
Na. Zuen Msuya, Pwani
0 Maoni