Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.
Dk Hussein Ali Mwinyi akimaliza ziara yake nchini Cuba, amekutana na Makamu wa
Rais wa Uganda Mhe. Jessica Alupo pamoja na ujumbe wa Wizara ya Kilimo ya Cuba
ikiongozwa na Naibu wa Wizara huyo Mhe. Bernado.
Rais Dk Mwinyi katika mazungumzo hayo alimshawishi Makamu
huyo wa Rais wa Uganda nchi yake ianze kutumia viuadudu, dawa inayotengenezwa
Kibaha, Mkoa wa Pwani, Tanzania na kiwanda kinachotumia teknolojia kutoka kwa
wataalamu wa Cuba kwa ajili ya kuangamiza vimelea vya mbu kwa lengo la
kuangamiza Malaria.
Mhe. Rais Dk. Mwinyi alimueleza Makamu huyo wa Rais wa
Uganda kwamba kiwanda hicho kilianza uzalishaji wa viuadudu tangu mwaka 2017.
Nchi kadha za Afrika zimenufaika na dawa hiyo ya viuadudu
kutoka Kibaha ikiwemo Niger, Angola, Msumbiji na Eswatini.
Dk. Mwinyi alimueleza Makamu Jessica Alupo kwamba mbali ya
kutengeneza viuadudu kiwanda hicho teknolojia yake kinaweza kutengeneza pia
mbolea.
Baada ya Maelezo hayo Makamu wa Rais wa Uganda alionesha
kuvutiwa na bidhaa hiyo na kueleza kwa vile nchi yake inasumbuliwa na Malaria
wapo tayari kutumia bidhaa hiyo itakayosaidia kuondokana na vifo vya watoto na
kina mama vinavyotokana na Malaria.
Kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Rais Dk.
Mwinyi aliahidi kuigaiya bure Uganda lita elfu moja za dawa hiyo waijaribu na
baadae wapeleke wataalam wao wa Afya kuangalia teknolojia ya kuzalisha dawa
hiyo ombi lililokubaliwa na Makamu wa Rais wa Uganda Jessica Alupo.
Naye Naibu Waziri wa Kilimo wa Cuba Mhe Bernado alieleza
wamesaidia kuingiza teknolojia ya dawa ya viuadudu ili kusaidia mapambano dhidi
ya Malaria Afrika.
Mazungumzo hayo pia yalihudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Steve Byabato na Balozi wa
Tanzania nchini Cuba Mhe. Humphrey Polepole.
0 Maoni