Afungwa jela miaka mitatu kwa kumwagia maji ya moto mke mwenza

 

Vumilia Kasomelo mkazi wa Buchosa wilayani Sengerema mkoani Mwanza amehukumiwa kwenda jela gerezani miaka mitatu kwa kosa la kumjeruhi kwa kummwagia maji ya moto mke mwenzake aitwaye Mariam, kisa wivu wa mapenzi.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Evod Kisoki wa Mahakama ya wilaya ya Sengerema baada ya mshtakiwa huyo kukiri kutenda kosa hilo

Awali akisoma shtaka hilo kwenye kesi namba 109 ya mwaka huu mwendesha mashtaka wa serikali Morice Mtoi amesema tukio hilo lilitokea tarehe 26 ya mwezi uliopita majira ya saa tatu usiku katika kijiji cha Lugata tarafa ya Buchosa wilayani Sengerema ambapo mshtakiwa huyo alimmwagia maji ya moto mke mwenzake alipokuwa amelala na kumsababishia majeraha.

Mwendesha mashtaka huyo wa serikali amesema Vumilia ametenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 225 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 toleo la mwaka 2022.

Mshtakiwa huyo baada ya kukiri kutenda kosa hilo Mahakama ikamhukumu kifungo cha miaka mitatu jela ili iwe fundisho kwa wengine watakaojaribu kufanya kosa kama hilo.


Mariam akiwa na majeraha ya kuuguzwa na maji ya moto na mke mwenza Vumilia Kasomelo, tukio ambalo limefanyika wakati wakiwa kwenye msiba wa baba mkwe wao.


Chapisha Maoni

0 Maoni