Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewasisitiza watumishi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Itigi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na
ubunifu ili tija ya kazi zao iweze kuonekana kupitia huduma bora wanazozitoa
kwa wananchi.
“Ninatamani kuona utendaji kazi wenu unazingitia misingi ya
maadili ya utendaji katika utumishi wa Umma kwani ndiyo msingi wa mageuzi
kuelekea maendeleo endelevu vinginevyo watumishi wazembe na wenye mienendo
isiyofaa kimaadili mwisho wao umefika,” alisisitiza Mhe. Ridhiwani.
Aidha, amewakumbusha watumishi hao kuwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anasisitiza uadilifu kazini
na ametoa haki na stahiki mbalimbali kwa watumishi, hivyo, Serikali kupitia
Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imekamilisha
mapitio, kusanifu na kuanza kujenga mifumo ya utendaji kazi Serikalini ili
dhana ya wajibu pia iweze kutekelezeka kwa ufanisi.
Pia, Naibu Waziri huyo amezitaka Mamlaka za Ajira na Nidhamu
kuendelea kusimamia haki na stahiki zote za watumishi na kuachana na kasumba ya
utendaji wa mazoea. Pia, amesema Mamlaka za Ajira na Nidhamu zirejee Sheria ya
Utumishi wa Umma, Sura ya 298 ambayo inaonesha kuwa madaraka kuhusu ajira,
kuthibitishwa kazini, mafunzo, kupandishwa cheo, nidhamu hadi hitimisho la kazi
kwa mtumishi wa umma yalishagatuliwa na hivyo kushindwa kutekeleza wajibu huo
ni kielelezo cha kushindwa kutekeleza majukumu waliyopewa.
Katika hatua nyingine Mhe. Ridhiwani amezitaka Halmashauri
nchini kuhakikisha zinaendeleza miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii- TASAF
kwa kuwa ni chaguo na imeridhiwa na wananchi wenyewe katika maeneo yao. Iwapo
Halmashauri na TASAF zitaunganisha nguvu ni rahisi kuwakomboa wananchi katika
umaskini.
“Ninaelekeza walengwa wote wenye sifa za kunufaika na TASAF
wasilipwe fedha nusu nusu kwa kuwa lengo ni kuwatoa katika wimbi la umaskini,”
alisema Mhe. Ridhiwani.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Mhe. Kemilembe Lwotta
ameomba pongezi zifike kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan kwa kuleta watumishi wapya wa kada mbalimbali 228 na wote
wameripoti kazini na watumishi 289 walimu na wasio walimu wamepandishwa vyeo na
15 wamebadilishiwa vyeo.
Vilevile, ameongeza kuwa wananchi katika Halmashauri ya Wilaya
ya Itigi katika vijiji vyote 39 wananufaika vyema na uwepo wa Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii- TASAF kwa kiwango kikubwa kwa kuwa kaya masikini zimefikiwa
na zinawezeshwa kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya
ya Itigi Bw. John Mgalula pamoja na shukurani alizotoa kwa Serikali, ameomba
Serikali kuendelea kutoa vibali vya ajira ili watumishi waongezeke na utoaji
huduma kwa umma uimarike.
Mhe. Ridhiwani amehitimisha ziara yake ya siku moja tarehe
25 Agosti, 2023 katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi iliyolenga kuhimiza
uwajibikaji kwa watumishi na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika
Halmashauri hiyo.
0 Maoni