WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea
kuyaenzi mambo yote mazuri yaliyofanywa na marehemu, Bernad Membe wakati wa
utumishi wake Serikalini.
Marehemu Membe ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje
alifariki dunia Mei 12 mwaka huu katika hospitali ya Kairuki jijini Dar es
Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.
Amesema marehemu Membe enzi za uhai wake alikuwa
mwanadiplomasia mahiri kwenye medani za Kitaifa na Kimataifa, hivyo Serikali na
Watanzania wataendelea kumkumbuka.
Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Agosti 26, 2023) aliposhiriki
ibada ya kumbukumbu ya marehemu Membe iliyofanyika nyumbani kwa marehemu Rondo,
Lindi.
Amesema weledi, nidhamu, uchapakazi na umahiri wa marehemu
Membe uliitambulisha Tanzania katika medani za kimataifa na kutengeneza
marafiki na mataifa mengine.
“Mheshimiwa Membe alikuwa na weledi wa kitaifa na kimataifa,
jumuiya za kimataifa zinatambua umahiri wake na alijizolea sifa kwa sababu ya
nidhamu na uchapakazi wake,” amesema Mhe. Majaliwa.
Naye, Waziri wa Habari na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye
akizungumza kwa niaba ya familia ya marehemu aliishukuru Serikali kwa
ushirikiano ilioutoa katika kipindi cha msiba.
“Namshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
kutoa zaidi ya shilingi milioni 100 kwa ajili ya ukarabati wa kanisa
ulioanzishwa na marehemu Membe, “amesema Mhe. Nape.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni