Kuelekea maadhimisho ya miaka 62 ya uhuru wa Tanzania Bara,
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kushirikiana na makampuni ya
waongoza watalii imepanga kuwapeleka watanzania katika kilele cha Mlima
Kilimanjaro lengo likiwa ni kusherehekea miaka 62 ya Uhuru, tukio hili la
kihistoria hufanyika kila mwaka ifikapo tarehe 9, Disemba.
Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara -TANAPA
Herman Batiho, amewaeleza wanahabari katika mkutano na Vyombo vya Habari Makao
Makuu ya TANAPA jijini, Arusha leo tarehe 28.08.2023 kuwa, Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) limekuwa na utaratibu wa kuadhimisha sherehe za Uhuru wa
Tanganyika tangu ulivyopatikana mwaka 1961. Maadhimisho haya yamekuwa
yakifanyika kwa kupandisha bendera ya nchi yetu katika kilele cha Mlima
Kilimanjaro. Tukio hili limekuwa likihusisha kikundi cha wanajeshi wachache
wakishirikiana na askari wa Hifadhi za Taifa Tanzania kwa utaratibu wa kampuni
ya utalii ya ZARA ambapo kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita maadhimisho
haya yalipata sura mpya ya ushiriki wa wananchi na kutambulika kwa jina la
“Twenzetu Kileleni” ambapo kwa sasa ni msimu wa tatu.
Aidha, Kamishna Batiho aliongeza kupitia hamasa kubwa na
mwamko wa watanzania wengi katika kipindi hicho ambapo Shirika la Hifadhi za
Taifa Tanzania limeongeza wigo kwa kushirikiana na mawakala wote wa utalii
kuratibu kampeni za twenzetu kileleni kwa lengo la kuendelea kuhamasisha utalii
wa ndani wakati wa maadhimisho ya Uhuru tarehe 9, Disemba. Lengo likiwa ni
kuongeza wigo wa utangazaji wa njia nyingi za kupanda Mlima Kilimanjaro na
fursa zaidi kwa watanzania kuchagua kampuni na njia wanazotaka kupanda mlima na
sio njia ya Marangu tu kama ilivyozoeleka.
“Kati ya kampuni zote tulizozialika kushiriki katika uratibu
wa maadhimisho haya ni kampuni tatu ndio zimejitokeza kushiriki kampeni hii
katika msimu huu wa tatu. Kampuni hizo ni ZARA, African Zoom na African Scenic,”
Alisema Kamishna Batiho.
Aidha, kampuni ya ZARA TOURS itatumia njia ya Marangu kama
ilivyozoeleka, African Zoom watatumia njia ya Machame na African Scenic
watatumia njia ya Lemosho ambapo idadi ya siku za kupanda mlima huo ni 6 kwa
njia ya Marangu, siku 7 kwa njia ya Machame na kwa Lemosho itakuwa siku 8
Gharama za kupanda mlima zitakuwa ni shillingi 1,150,000/- kwa njia ya Marangu,
shillingi 1,400,000/- kwa njia ya Machame na 1,700,000/- kwa njia ya Lemosho
aliongeza Kamishna Batiho.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya
Taifa Kilimanjaro Angela Nyaki alitoa rai kwa watanzania wote kushiriki
kuadhimisha sherehe hizo za uhuru katika kilele kirefu zaidi barani Afrika.
“Kama mwenyeji wa mlima niwakaribishe watanzania wa mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani kuja kushiriki nasi katika sherehe hizi za Uhuru katika Paa la Afrika. Nina imani watanzania wengi wana shauku kubwa ya kushiriki haya maadhimisho, kwa kulipa kidogo kidogo na kwa wale watanzania wenzetu ambao wamewahi kupanda kwa njia ya marangu nitoe wito sasa tuhamie njia nyingine ili tuuone mlima wetu kwa upande mwingine pia,” alisema Kamishna Nyaki.
Na. Edmund Salaho- Arusha
0 Maoni