Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) linafanya jitihada
mbalimbali za kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini nchini kwa kuwapatia
elimu pamoja na kuwanunulia mitambo ya kisasa ya uchimbaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO CPA, Dkt. Venance Mwasse,
amesema katika utafiti walioufanya wamebaini wachimbaji wadogo wanakabiliwa na
ukosefu wa taarifa sahihi za mashapo, teknolojia duni, kutokuwa na
mitaji/kutokopesheka na kukosa masoko.
Akiongea na Wahariri leo, CPA, Dkt. Mwasse amesema STAMICO
imenunua mitambo mitano ya kufanyia uchorongaji maalum kwa ajili ya wachimbaji
wadogo, na kuongeza kwamba mitambo hiyo inatarajiwa kufika nchini mwezi Septemba
2023.
"Licha ya kununua mitambo hiyo mitano ya uchorongaji
kwa wachimbaji wadogo, pia STAMICO itafanya ununuzi wa mitambo mingine 10,
ambapo ifikapo mwishoni mwa mwaka wa fedha 2023/24 jumla ya mitambo 15 itakuwa
imenunuliwa," amesema CPA, Dkt. Mwasse.
Ameongeza kuwa STAMICO itaanzisha vituo vya mfano vya
kujifunzi teknolojia vyenye tija ya uchimbaji katika maeneo ya Lwamgasa,
Katente na Itumbi, ambavyo vitawasaidia wachimbaji wadogo.
Akiongelea mafanikio ya STAMICO CPA, Dkt. Mwasse amesema
kwamba wamefanikiwa kuongeza mapato ya ndani kutoka shilingi bilioni 1.3 kwa
mwaka 2018/19 hadi kufikia shilingi bilioni 61.1 kwa mwaka 2022/23.
Pamoja na mambo mengine amesema kuwa shirika hilo
limefanikiwa kutoka katika kujiendesha kwa hasara hadi kujiendesha kwa faida na
kufanikisha kulipa gawio la serikali la jumla ya shilingi bilioni 8, na
kuondoka kabisa katika utegemezi.
0 Maoni