Serikali itaendelea kushirikiana na wadau ili kuhakikisha
wanawake wanapata fursa mbalimbali za kujikwamua kiuchumi na kuendeleza
biashara zao.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima alipokuwa akizindua
Programu ya kuwawezesha wanawake kiuchumi ijulikanayo kama Women Empowerment
Program (WEP) inayosimamiwa na kuratibiwa na Benki ya EXIM Tanzania, katika
hafla iliyofanyika Agosti 28, 2023 jijini Dar Es Salaam.
Waziri Dkt. Gwajima amesema uchumi unapoimarika ndivyo
familia inakuwa na ustawi bora na kupunguza madhira ya vitendo vya ukatili
kwenye familia.
“Kwa takwimu tulizonazo, takriban asilimia 70 ya wanawake
bado wapo kwenye ajira zisizo rasmi wakijishughulisha na biashara ndogo ndogo
kama mama ntilie na kazi za nyumbani. Kwa mfano, kwa mujibu wa takwimu za
Finscope za mwaka 2017, kati ya watu 3,014,106 waliokuwa kwenye ajira rasmi
wanawake walikuwa 1,107,917 sawa na asilimia 36.8 tu,” alisema Waziri Dkt.
Gwajima
“Ni matumaini yangu kuwa programu hii ya WEP ya Benki ya
Exim imekuja muda muafaka na itakuwa chachu ya kupunguza pengo ili na kuwafanya
wanawake washiriki kikamilifu katika sekta ya kifedha,” alisisitiza Waziri Dkt.
Gwajima
Katika hatua nyingine Waziri Dkt. Gwajima ameipongeza Benki
ya Exim Tanzania kupitia mpango huo, kwa kutoa mkopo bila riba wa dola elfu
kumi (takribani shilingi milioni 25) kwa wahitimu watatu bora kwa kipindi cha
miaka mitatu na kusema jitihada hizo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za
kuwawezesha wanawake kiuchumi.
Akieleza juhudi za Serikali juu ya kuwawezesha wananchi hasa
wanawake kiuchumi Waziri Dkt. Gwajima amesema Serikali imeanzisha jumla ya
Mifuko 61 ya Uwezeshaji wa Wananchi
Kiuchumi na hadi sasa imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni
2.22 kwa wanawake millioni 5.3 na mwaka 2018, Serikali ilipitisha sheria ambayo
ilizielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga asilimia 10 ya mapato ya
ndani kwa ajili ya kutoa mikopo isiyo na riba (Wanawake 4%, Vijana 4% na Watu
wenye Ulemavu 2%).
“Tangu kipindi hicho, mikopo yenye thamani ya zaidi ya
shilingi bilioni 63.489 imetolewa na kuwanufaisha wanawake zaidi ya 938,800”.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim Jaffari
Matundu amesema Benki hiyo imefanikiwa kushirikiana na wadau wengine katika
kuwezesha wanawake kiuchumi kwa kuwapatia fursa za kupata mikopo isiyo na riba
ambayo imewasaidia kupata mitaji na kuongeza vifaa vya uzalishaji hivyo
kuongeza masoko kwa ajili ya bidhaa zao.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Ndoto Hub, Faraja Nyarandu
amesema kuwa mpaka sasa kwa kushirikiana na Benki ya Exim wameweza kuwafikia
wanawake 63,000 katika kuhakikisha wanawake wanapata fursa za kuendeleza ndoto
za biashara zao kwa kupata mitaji na masoko ili kupata mafanikio katika
biashara zao.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi
Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akikabidhi cheti kwa mmoja wa wahitimu wa
mafunzo yaliyotolewa na Benki ya Exim kwa Wanawake wajasirimali katika hafla
iliyofanyika Agosti 28, 2023 jijini Dar es Salaam.
Na WMJJWM- Dar Es Salaam
0 Maoni