Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kiwango cha thamani ya uwekezaji Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) imeongezeka hadi kufikia shilingi trilioni 7.98 kwa mwaka 2022/2023 kutoka shilingi trilioni 7.5 kwa hesabu za mwaka wa fedha ulioishia Juni, 2022.
Amesema hayo leo (Jumamosi, Agosti 12, 2023) wakati wa
maadhimisho ya miaka mitano ya mfuko huo na uzinduzi wa huduma za wanachama
kidijitali, kwenye ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma.
“Thamani hii ipo katika soko la hisa ambalo ni kichocheo
kikubwa katika ukuaji wa mitaji nchini ambapo mfuko huo ni muwekezaji mkubwa wa
ndani mwenye hisa katika makampuni makubwa kama CRDB Bank Plc, NMB Bank Plc,
Tanzania Breweries Limited, na Vodacom Tanzania Plc.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ameitaka Mifuko ya Hifadhi ya
jamii kufanya uwekezaji wenye tija kwa wanachama na jamii inayolingana na
thamani ya fedha za wanachama “Fanyeni utafiti wa kina kubaini masoko ili
uwekezaji unaofanywa usilete hasara kwa mifuko.”
Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza mifuko yote ya Hifadhi ya
Jamii kuendelea kulipa mafao kwa wakati ili kuleta utulivu kwa wanachama.
“Wazee wastaafu wasisumbuliwe, kumbukeni kuwa sisi sote ni wastaafu watarajiwa.”
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ameziagiza
taasisi za Serikali kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan alilolitoa wakati uzinduzi wa mkongo wa mawasiliano wa 2Afrika na
matumizi ya teknolojia ya 5G la kutaka taasisi zote za Serikali ziwe zinasomana
ili kurahisisha na kuboresha utoaji wa huduma kwa Watanzania.
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana,
Ajira na Wenye Ulemavu Prof Joyce Ndalichako amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt
Samia Suluhu Hassan kwa maono na dhamira ya dhati ya kuimarisha sekta ya
hifadhi ya jamii “lengo la Rais Samia ni kuona inafanya kazi kwa tija, ufanisi
na kutoa huduma bora. *
“Tunampongeza pia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwa uthubutu wa
kutoa fedha kwa mfumo wa hati fungani shilingi trilioni 2.17 za kulipa deni
ambalo lilimedumu kwa muda mrefu, mfumo huu umewezesha PSSSF kulipa wastaafu
kwa wakati.”
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii
kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) CPA Hosea Kashimba amesema kuwa kwa kipindi cha
miaka mitano, hadi kufikia Juni, 2023 mfuko huo umelipa kiasi cha shilingi
trilioni 8.88 kwa wanufaika 262,095.
Amesema kuwa kati ya
Julai, 2018 na Juni, 2023 mfuko huo umeweza kulinda na kuongeza thamani yake
kwa asilimia 27.76 kutoka trilioni 5.83 hadi trilioni 8.07 Juni, 2023.
“Ongezeko hili ni sawa na wastani wa asilimia 6.72 kwa kila mwaka”.
0 Maoni