Teknolojia ya 5G itarahisisha utoaji wa huduma- Samia

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu Hassan, ameiagiza Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhakikisha mifumo yote ya TEHAMA inasomana na taasisi zinazosimamia sera hizo.

Rais Samia ametoa agizo hilo leo wakati wa uzinduzi wa mkongo wa mawasiliano wa 2Afrika na matumizi ya teknolojia ya 5G iliyofanyika katika ofizi za kampuni ya Airtel zilizopo eneo la Tanki Bovu, Dar es Salaam.

Aidha, Rais Samia amesema msingi imara kwenye TEHAMA na mifumo ya mawasiliano kisera, kisheria na kitaasisi itawezesha kujenga uchumi jumuishi wa kidigitali (digital Inclusive economy) na kuinua maisha ya wananchi wa mjini na vijijini.

Vile vile, Rais Samia amesema uzinduzi wa teknolojia ya 5G itarahisisha utoaji wa huduma mbalimbali ikiwemo utunzaji wa taarifa muhimu, ukusanyaji wa maduhuli ya serikali, kutuma na kupokea fedha pamoja na biashara za mitandaoni.

Pamoja na mambo mengine, Rais Samia amesema kuwa kuongezeka kwa mkongo huo kutatoa fursa kwa mitandao ya simu na watoa huduma wengine kuchagua mkongo wanaotaka kutumia, hivyo kuongeza ubora na kushusha gharama za intaneti

Mkongo wa 2Afrika unaunganisha bara la Asia, Ulaya na Afrika kwa urefu wa kilometa 45,000 na kutumiwa na zaidi ya watu bilioni 3 duniani.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza kwa njia ya Mtandao na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Mkongo wa Baharini cha Airtel 2Afrika pamoja na Mtandao wenye kasi ya 5G wa Kampuni ya Mawasiliano ya Artel Tanzania iliyofanyika Mbezi Tanki Bovu Jijini Dar es Salaam tarehe 10 Agosti, 2023.


Chapisha Maoni

0 Maoni