SERIKALI imeendelea kutoa elimu ya kanuni mpya ya mafao ya
pensheni (kikokotoo) na hadi Juni 30, mwaka huu wanachama wa mifuko ya pensheni
131,497 na waajiri 5,580 wamefikiwa na elimu hiyo.
Adha, Elimu hiyo imetolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya
Jamii (NSSF), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa
kushirikiana na Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na
Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi amebainisha hayo bungeni Agosti 29, 2023
alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Moshi Mjini (CCM), Mhe. Priscus
Tarimo aliyetaka kujua mpango wa serikali kuhusu malalamiko ya wastaafu juu ya
kikokotoo kinachotumika kupiga mahesabu na kulipa mafao.
Mhe. Katambi amesema mpango wa serikali ni kuendelea
kuwaelimisha wananchi hususani waajiri na wanachama wa mifuko hiyo wakiwamo
wastaafu kuhusu faida ya kanuni hizo.
Amesema kwasasa kwenye mkupuo wa malipo wanufaika asilimia
81 ya wanachama wote na asilimia 19 mafao yao ya kila mwezi yameongezeka
kupitia kanuni hizo.
“Katika malipo yale ya kila mwezi kulikuwa kuna asilimia 50
walikuwa wanalipwa lakini sasa wamefikia asilimia 67 ya malipo, haya maboresho
yametokana na utafiti uliofanyika na utaratibu wa kuunganisha mifuko ya
pensheni imeleta tija kubwa,” amesema Mhe. Katambi.
0 Maoni