Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema Serikali inaendelea na jitihada za
kumaliza changamoto ya magugu maji kuzingira Ziwa Jipe wilayani Mwanga Mkoa wa
Kilimanjaro.
Amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mwanga Mhe.
Joseph Tadayo aliyetaka kujua lini Serikali itatekeleza mradi wa kuondoa magugu
maji katika Ziwa Jipe.
Dkt. Jafo amesema Ofisi hiyo kupitia Baraza la Taifa la
Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) tayari zimefanya tathimini ya
uharibifu uliopo na kuandaa andiko la Mradi wa Hifadhi ya Ardhi, na vyanzo vya
maji.
Akiendelea kujibu swali hilo amebainisha kuwa jumla ya Dola
za Marekani milioni sita ambazo ni sawa na takriban shilingi bilioni 15 zinatarajiwa
kupatikana kupitia mradi huo.
“Serikali imeona changamoto ya uharibifu wa Mazingira
unaotokana na kuenea kwa magugu maji katika Ziwa Jipe, hadi sasa jitihada za
kutafuta fedha kutoka kwa wafadhili mbalimbali zinaendelea,” amesema Mhe. Jafo.
Amefafanua kuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha inarejesha
ikolojia ya ziwa hilo ili kuleta manufaa kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo
pamoja na uhifadhi wa mazingira.
Aidha, Waziri Dkt. Jafo ameongeza kwa kusema kuwa Serikali
itahakikisha inatekeleza mradi huo mara baada ya fedha kupatikana ili
kuwanusuru wananchi wa eneo dhidi ya athari za magugu maji hayo.
Pamoja na majibu hayo pia Waziri Jafo ametoa wito kwa
wananchi kuendelea kuhifadhi mazingira katika Ziwa Jipe ikiwemo kuacha kufanya
shughuli za kibinadamu zisizo endelevu.
Ziwa Jipe lina ukubwa wa kilomita za mraba 30 na linahudumia
wananchi zaidi ya 3,000 wanajishughulisha na shughuli za uvuvi, kilimo, ufugaji
na uhifadhi wa bionuwai pamoja na shughuli za utalii.
Hata hivyo inaelezwa kuwa shughuli za uvuvi zimeathiriwa kwa
kiasi kikubwa na kukithiri kwa magugu maji yaliyoota ziwani hasa upande wa
Tanzania hivyo Serikali inaendelea na jitihada za kuondoa magugu maji hayo.
0 Maoni