Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), umelipa
kiasi cha shilingi bilioni 35 kwa waliokuwa watumishi wa umma zaidi ya 13,000,
waliofukuzwa kazi katika sakata la vyeti feki, ambao malipo yao yametokana na
huruma ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa watumishi hao.
Rais Samia Suluhu Hassan alitoa agizo hilo katika Siku ya
Wafanyakazi Duniani Mei Mosi ya mwaka 2022, ambapo aliagiza kuwa walioondolewa
kwa vyeti feki enzi ya Serikali ya Awamu ya Tano walipwe stahiki zao kama mafao
ya kustaafu, kwa kuwa watumishi hao waliutumikia umma.
Hayo yameelezwa leo na Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF CPA Hosea
Ezekiel Kashimba, katika mkutano wake na Wahariri wa Vyombo vya Habari alipokuwa
akielezea mafanikio ya PSSSF ndani ya miaka mitano, na kusema mfuko huo umebeba
dhamana hiyo kwa kuwa waliofukuzwa kazi walikuwa ni watumishi wa umma.
“Katika kipindi cha miaka mitano PSSSF imefanya malipo ya
mafao yanayofikia kiasi cha shilingi trilioni 8.88 kwa wanachama wake, kwa njia
ya mafao mbalimbali yakiwemo malipo ya uzeeni, pensheni ya kila mwezi, mafao ya
kifo, fao la kuacha kazi pamoja na mafao mengine,” amesema CPA Kashimba.
CPA Hosea pia amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa
kuidhinisha Serikali kulipa shilingi trilioni 2.17 ambayo ni malipo ya
malimbikizo ya michango ya wanachama wa kabla ya Mwaka 1999 ya uliokuwa Mfuko
wa PSPF, kati ya shilingi trilioni 4.6.
“Katika utekelezaji wa kipindi cha miaka mitano PSSSF
imekusanya michango ya jumla ya shilingi trilioni 9.60, kiasi hiki
kinajumuisha shilingi trilioni 2.17 ambayo ni malipo ya malimbikizo ya michango
ya wanachama wa kabla ya mwaka 1999 ya uliokuwa Mfuko wa PSPF,” amesema CPA
Kashimba.
Kuhusu uwekezaji unaofanywa na PSSSF CPA Kashimba amesema thamani
ya uwekezaji imeongezeka kwa asilimia 23.5, kutoka shilingi trilioni 6.40 hadi kufikia
shilingi trilioni 7.92, sawa na ongezeko la wastani wa 4% kwa mwaka.
Amesema mafanikio ambayo mfuko wa PSSSF umeyapata kwa kiasi
kikubwa yamechangiwa na nia ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya
uongozi mahiri wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais ya Jamhuri wa Muungano wa
Tanzania.
CPA Kashimba ametumia mkutano huo kwa niaba ya Bodi ya
Wadhamini wa Mfuko, kumshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, kwa uthubutu wake
wa kuamua kulipa deni la michango la shilingi trilioni 4.6 la wanachama wa
uliyokuwa Mfuko wa PSPF ya kabla ya Mwaka 1999, uamuzi ambao umewezesha Mfuko
kulipwa kiasi cha shilingi trilioni 2.17 kupitia hatifungani maalum.
Serikali pia imelipa shilingi bilioni 500 katika deni la
shilingi bilioni 731.4 la mikopo ya miradi ambayo mifuko iliyounganishwa
iliikopesha Serikali ili kutekeleza miradi ikiwemo ujenzi wa; Jengo la Bunge,
Chuo Cha Serikali cha Hombolo, Nelson Mandela Istitute of Science and
Technology na Chuo Kikuu cha Dodoma.
Kuhusu uamuzi wa kuunganisha mifuko, CPA Kashimba amesema
kwamba umekuwa wa manufaa kwa mfuko wa PSSSF, kwa kuuwezesha kujiendesha kwa
ufanisi na kulipa mafao ya wanachama wake kwa wakati kutokana na kuongezeka kwa
thamani ya mfuko.
0 Maoni