Muhimbili yaanza kutibu kiharusi, wagonjwa wanapona na kutembea

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi amesema hospitali hiyo imeanza kutumia mtambo maakum wa kuyeyusha damu iliyoganda kwa mtu aliyepata ugonjwa wa kiharusi.

Profesa Janabi amesema hayo jana Jijini Dodoma, na kuongeza kuwa kwa sasa watu wanaopata ugonjwa wa kiharusi nchini wanatibiwa kwenye kifaa hicho na wanauwezo wa kupona na kutembea kama kawaida.

“Ukipata kiharusi sasa hivi kama upo Dar es Salaam, ukiletwa Muhimbili tuna uwezo wa kukuingiza kwenye mtambo na kutoa hiyo damu iliyoganda na ukapata nguvu na ukatembea kama zamani,” alisema Prof. Janabi na kuongeza, “Haya ni maendeleo makubwa maana tutapunguza ulemavu kwa wagonjwa hao”.

Profesa Janabi ambaye alikuwa akiongea kwenye mkutano wake na waandishi wa habari, amesema mtambo huo pia unatumika kutibu wagonjwa watakaokuwa na tatizo la mishipa ya miguu kuziba.

“Kwa kutumia mtambo huo pia tutatibu kina mama walio na uvimbe kwenye mfuko wa uzazi hatutakuwa na haja ya kufanya upasuaji tunaweza kuyeyusha uvimbe kwenye mashine,” alisema Prof. Janabi.

Kwa upande wa wagonjwa wa saratani, Profesa Janabi amesema badala ya kupiga dawa ya saratani mwili mzima mtambo huo pia unauwezo wa kugundua tatizo lilipo na kutibu eneo husika lililokuwa na saratani.

 “Ukitumia dawa za saratani mwili mzima kuna madhara pia lazima upate sasa mtambo utarahisisha madhara ya dawa itakuwa kidogo, sisi umeshaanza kuufanyia kazi huduma zipo zinapatikana katika hospitali yetu ya taifa,” alisema Prof. Janabi.

Chapisha Maoni

0 Maoni