Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mohamed Mchengerwa leo
tarehe 24 Agosti, 2023 amewaaga rasmi wananchi kutoka eneo la Hifadhi ya
Ngorongoro ambao ni awamu ya pili ya waliojiandikisha kuhama kwa hiari kwenda
maoneo mbalimbali nje ya Hifadhi.
Kundi hilo la Wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro lililoagwa
leo linajumuisha kaya 16 na zenye wananchi 87 na mifugo 740 ambapo kati ya kaya
hizo, kaya 14 zinahamia katika maeneo ya Wilaya za Monduli, Karatu na Arusha
ziliko Mkoa wa Arusha na kaya 2 zinahamia Kijiji cha Msomera Handeni Mkoani
Tanga.
Akiaga kundi hilo Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mohamed
Mchengerwa ameeleza kuwa Serikali katika awamu ya pili ya utekelezaji wa zoezi
hili linaenda sambamba na ujenzi wa nyumba 5,000 za makazi katika maeneo ya
Serikali yaliyopo Msomera Wilayani Handeni na eneo la Kitwai lililopo Wilaya ya
Kilindi.
Ameongeza kuwa katika awamu hii ya pili ya utekelezaji wa
zoezi Serikali imewapa uhuru wananchi kuhamia katika maeneo yaliyoandaliwa na
serikali au maeneo yoyote ambayo mwananchi atachagua mwenyewe na serikali
itakuwa tayari kuwapa stahiki zao kwa mujibu wa sheria na kusafirisha mali zao
ikiwemo samani na mifugo.
Akitoa taarifa kuhusu wanaohama Naibu kaamishna wa Uhifadhi
NCAA Elibariki Bajuta ameainisha kuwa katika awamu ya kwanza iliyoishia mwezi
Januari 2023 jumla ya kaya 547 zenye watu 3,010 na mifugo 15,321
zilikwishahamia kwa hiari katika Kijiji cha Msomera na maeneo mengine kwa ajili
ya kupisha shughuli za Uhifadhi.
Amebainisha kuwa awamu ya pili ya ujenzi wa nyumba 5000
unaoanza hivi karibuni utaenda sambamba na ujenzi wa miundombinu ya kijamii
ikiwepo barababara, vituo vya Afya, zahanati, maji, umeme, majosho, malambo na
kituo cha polisi kwa ajili ya usalama wa wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mhe. Mwl Raymond Mangwala
ameeleza kuwa kwa sasa zoezi la uelimishaji, uandikishaji na uthaminishaji
linaendelea na wale wote watakaohamishwa kwenda maeneo mbalimbali, Serikali
itaendelea kuwalipa stahiki zao zote kwa mujibu wa sheria na kufuata misingi ya
haki za binadamu.
Na Kassim Nyaki, NCAA.
0 Maoni