Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesisitiza kuwa maslahi ya watumishi
ni kipaumbele katika awamu hii ya Sita ili kuongeza motisha na kuchochea zaidi
utendaji kazi na utoaji wa huduma bora kwa umma.
Mhe. Ridhiwani amesema na kusisitiza hayo tarehe leo alipokuwa
akizungumza na viongozi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Singida katika ofisi hizo.
“Kila mara tunaona Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akitangaza kutoa haki na stahiki mbalimbali kwa
watumishi wa umma, hivyo, kila mmoja wetu kwa nafasi yake anatakiwa pia
kuwajibika ipasavyo ili kuleta ufanisi zaidi” ameongeza Mhe. Ridhiwani.
Aidha, amewakumbusha watumishi hao kutoka ofisini na kwenda
kuwahudumia wananchi na kutatua changamoto zilizo ndani ya uwezo wao.
Katika hatua nyingine Mhe. Ridhiwani ametembelea na kukagua
ujenzi wa majengo ya Chuo cha Utumishi wa Umma, Kampasi ya Singida awamu ya
pili inayohusu majengo ya madarasa na vyoo vya nje na kuelekeza viongozi
kuhakikisha miundombinu ya watu wenye ulemavu inazingatiwa katika ujenzi huo.
“Chuo cha Utumishi wa Umma ni muhimu sana kwa kuwa kinaandaa
watumishi wa umma bora na ambao ni msingi wa maendeleo ya nchi katika nyanja
zote” ameongeza Mhe. Ridhiwani.
Vilevile, akiwa katika ziara ya kutembelea wanufaika wa
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii- TASAF katika Kijiji cha Ughaugha Kata ya Unyamikumbi,
Manispaa ya Singida amesema Serikali imetoa zaidi ya bilioni 51 kwa ajili ya
kunusuru kaya maskini nchini ili ziweze kuboresha maisha yao mathalani kwa
kupata chakula milo 3 kwa siku, kusomesha watoto na kupata huduma za matibabu
kwenye vituo vya afya na zahanati.
Naye, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Bw. Stanislaus
Choaji amesema wamepokea maelekezo na watahakikisha wanatazama kwa jicho pevu
maeneo ya pembezoni katika Mkoa wa Singida kwa kutoa na kupanga watumishi ili
kuboresha utoaji wa huduma kwa umma.
Aidha, Bw. Choaji ameongeza kuwa wananchi wa Mkoa wa Singida
wananufaika na uwepo wa TASAF kwa kuwa kaya maskini ambazo ni wanufaika
wamepata fedha na wanafanya shughuli za kiuchumi ikiwemo kufuga Mbuzi, Kuku na
Kondoo kwa ajili ya kujikwamua katika wimbi la umaskini, hivyo salamu za
shukurani zimfikie Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ukombozi huo.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu, Chuo
cha Utumishi wa Umma Dkt. Ernest Mabonesho amesema ujenzi umefikia asilimia 21
na kazi inayoendelea ni ujenzi wa kuta ambapo hadi sasa mradi huo umetoa ajira
za vibarua kwa wananchi 96 wanaozunguka eneo la mradi ikiwa wanaume ni 62 na
wanawake ni 34.
Mhe. Ridhiwani amehitimisha ziara yake ya siku mbili katika
Mkoa wa Singida ambapo alianzia Halmashauri ya Wilaya ya Itigi na kumalizia
katika Manispaa ya Singida. Ziara hiyo ililenga kuhimiza uwajibikaji kwa
watumishi na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Mkoa huo
0 Maoni