Baba jela miaka 5 kwa kumuunguza mikono mwanaye mdokozi

 

Mkazi wa Chamagati Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza, Maneno Thomas (35) amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka mitano jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la ukatili dhidi ya mtoto wake.

Hukumu hiyo imetolewa leo Agosti 18, 2023 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Sengerema, Evod Kisoka ambaye alisema Mahakama baada ya kujiridhisha na ushahidi katika shauri hilo bila shaka imemkuta mshitakiwa na hatia ya ukatili dhidi ya mtoto wake.

Awali, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Morice Mtoi aliieleza mahakama hiyo kuwa Julai 30, 2021, mshtakiwa Thomas alitekeleza ukatili huo wa kummwagia maji ya moto mikononi, Daniel Maneno (8) katika kijiji cha Chamagati wilayani Sengerema mkoani Mwanza.

Mtoi alisema mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 169 (A) (1) na (2) cha Sheria ya Kanuni ya adhabu sura ya 16 toleo la mwaka 2022.

Hata hivyo, mshitakiwa alipopewa nafasi ya kujitetea kuhusu shtaka linalomkabili, mbali na kukiri pia, aliomba Mahakama impunguzie adhabu kwani mtoto wake alikuwa ni kero hata kwa majirani kutokana na vitendo vyake vya udokozi.

Hata hivyo Mahakama imetupilia mbali ombi hilo na kumuamuru kutumikia kifungo hicho ili iwe funzo kwa watu wengine.

Chapisha Maoni

0 Maoni