WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema uwekezaji una faida na kwamba suala hilo siyo kitu kipya.
“Uwekezaji una faida, hata hapa mbele yetu (jirani na eneo la
mkutano) kuna eneo la bandari limekodishwa na mtu ameweka uzio. Hawa watu
wanakodisha maeneo na wanayalipia,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo jana jioni wakati akizungumza na mamia
ya wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Bandari, mjini
Mtwara.
Amesema mwekezaji wa kwanza kwenye bandari ya Dar es Salaam
ambako uwekezaji unapigiwa kelele, mkataba wake ulikuwa na vipengele vyenye
mapungufu, vikaboreshwa mwaka 2017 na akaongezewa miaka mitano.
Akifafanua kuhusu makubaliano baina ya Serikali ya Tanzania
na Dubai kupitia kampuni ya DP World,
Waziri Mkuu amesema: “Ili mradi mmesema mkataba uzingatie maslahi ya Taifa,
tutahakikisha mkataba huo unazingatia maslahi ya Taifa. Mmekuwa na hofu na
ajira, hakuna atakayepoteza ajira. Mmekuwa na hofu na ardhi, kwamba anayekuja
atachukua ardhi, siyo kweli. Hakuna mwekezaji aliyepewa ardhi kwa sababu hata
kwenye sheria za uwekezaji, mwekezaji hapewi ardhi bali anapata kibali cha
kukaa juu ya ardhi, na analipa kodi.”
“Hofu nyingine ni muda wa mkataba, mmesema atakaa miaka 100.
Hapana, haijatamkwa popote ila akija tutakubaliana miaka ya kukaa na kufanya
tathmini kadri tunavyoona ukaaji huo utakuwa na maslahi ya Watanzania.”
Amesema kampuni ya DP World imewekeza kwenye nchi nyingi
duniani na imejenga bandari kavu nchini Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya
Congo. “Mwekezaji huyu anahudumia bandari zaidi ya 168 duniani, ana meli zaidi
ya 400. Meli hizi zitaleta mizigo kwenye bandari yetu. Ninawaomba Watanzania
tumwamini Rais wetu, ana nia njema sana ya kiuchumi ya kufungua milango.”
Mapema, Waziri Mkuu Majaliwa alitembelea bandari ya Mtwara na
kukagua utendaji kazi wake ikiwemo gati mpya, flow meter na matenki ya
kuhifadhia mafuta yanayomilikiwa na kampuni za GM na OILCOM.
Akiwa bandarini, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele
Mwakibete alimweleza Waziri Mkuu kwamba ujenzi wa gati mpya yenye urefu wa mita
300 umekamilika. “Gati hii ina uwezo wa kuhudumia meli hadi yenye uzito wa tani
65,000. Tumeongeza kina cha bandari hadi kufikia mita 13 na kazi yote
iligharimu sh. bilioni 157.”
“Hivi sasa bandari hii ina uwezo wa kuhudumia tani milioni moja za mizigo kwa mwaka kutoka 400,
000 kabla ya maboresho. Mwaka 2021/2022 kabla ya ujenzi wa gati hili, tulikuwa
tunakusanya sh. bilioni 5 lakini mwaka fedha ulioisha wa 2022/2023, tumeweza
kukusanya sh. bilioni 35.59. Tulikadiria kupokea meli 102 lakini tumeweza
kupokea meli 313,” alisema.
Naye Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara, Bw. Norbert Kalembwe
alisema bandari hiyo imenunua mashine mpya ya kupakua makontena kwenye meli kwa
thamani ya sh. bilioni 90.
Alisema tangu Aprili mwaka huu hadi sasa, wamepokea makontena
4,600 yakiwemo yenye uwezo wa kuhifadhi vyakula ambayo yakifika bandarini hapo,
yanaunganishwa na chaja za umeme ili kuendelea kutunza ubaridi uliomo ndani ya
makontena hayo.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema wanaomiliki vituo vya
mafuta Mtwara, Lindi na Ruvuma wanunue mafuta hayo kutoka Mtwara ili kuongeza
kasi ya uchumi kwenye bandari hiyo.
“Nimeenda kwenye depot za GM na Oilcom, hawa ndugu zetu
wamewekeza pale na tumewakodisha. Leo wamelalamika kuwa wauzaji wa rejareja
hawachukui mafuta kutoka Mtwara.”
“Wanaomiliki vituo vya mafuta kwenye mikoa ya Mtwara, Lindi
na Ruvuma hawana sababu ya kwenda Dar es Salaam kuchukua mafuta. Waje
wachukulie Mtwara ili bandari yetu na yenyewe iwe inaleta meli za mafuta.
Tusipofanya hivyo, tunaifanya bandari yetu isifanye kazi. Kama nilivyoagiza
Tanga, Waziri mwenye dhamana akae na waliojenga matenki kwenye bandari ya
Mtwara ili kuweka utaratibu ambao utawawezesha kufanya biashara. Hii itaongeza
mzunguko wa fedha kwa wana-Mtwara.”
0 Maoni