Dkt Mabula alisema hayo tarehe 12 Julai 2023 wakati akikagua
ujenzi wa mradi wa nyumba unaojulikana kama Samia Housing Scheme unaotekelezwa
na Shirika la Nyumba la Taifa kwenye eneo la Kawe jijini Dar es Salaam.
‘’Tunahitaji kujenga nyumba siyo tu kwa kutumia matofali
tuliyo nayo bali kuwa na teknolojia nyingine itakayotuwezesha ujenzi wa nyumba
nyingi na kwa muda mfupi lakini nyumba imara,’’ alisema Dkt Mabula.
Kwa mujibu wa Waziri Mabula, nchi zilizoendelea ziko kwenye
hatua nzuri kwa kuwa ndani ya mwezi mmoja zinaweza kujenga nyumba ishirini na
NHC inatakiwa kupiga hatua kwa kuangalia mabadiliko hayo.
Hata hivyo, Dkt Mabula alisema, mwaka ujao wa 2024 Tanzania
itakuwa mwenyeji wa maonesho ya kimataifa ya tekonolojia ya ujenzi wa nyumba za
gharama nafuu ambapo Tanzania itaweza kujifunza kutoka kwa wengine.
Aidha, Waziri Mabula alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuliwezesha Shirika la Nyumba la Taifa
kukopa fedha za kuendelea na miradi iliyosimama kwa muda mrefu.
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan iliruhusu Shirika la NHC
kukopa shilingi bilioni 173.9 ambapo hadi sasa Shirika limekopa bilioni 44.7
kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Akielezea zaidi kuhusu uhitaji wa nyumba nchini, Dkt Mabula
alisema kuwa, katika sensa iliyopita takwimu zinaonesha upo uhitaji wa zaidi ya
nyumba milioni 3.8 na kama ujenzi utafanyika kwa kasi basi zitahitajika
kujengwa nyumba laki tano kwa mwaka.
‘’Bado kuna uhitaji mkubwa wa nyumba na sehemu kubwa ya
nyumba zinazojengwa na Shirika letu la NHC watu wameonesha nia ya kuzichukua na
kwa mujibu wa sensa iliyopita upo uhitaji mkubwa wa nyumba katika jiji la Dare
es Salaam,’’ alisema Dkt Mabula.
Hata hivyo, alisema, habari njema ni kuwa, kupitia Bajeti ya
2023/2024 wananchi sasa wanaoenda kununua nyumba za gharama nafuu wameondolewa
Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) hivyo nyumba ya milioni 50 kushuka chini
itanunuliwa bila VAT.
Kufuatia hatua hiyo, Dkt Mabula aliweka bayana kuwa,
inachofanya serikali ni kuhakikisha nyumba za aina hiyo zinajengwa kwa wingi
ili watanzania waweze kununua. Ametoa rai kwa watu wenye fursa ya kuendeleza
ujenzi kufanya hivyo kwa kuwa uhitaji wa nyumba bado ni mkubwa.
Shirika la Nyumba na Taifa (NHC) lilibuni mradi wa nyumba
5000 za gharama nafuu wa Samia Housing Scheme zitakazojengwa kwa awamu katika
mikoa mbali mbali nchini kwa gharama ya shilingi bilioni 466. Kwa kuanzia,
Shirika lilianzisha ujenzi wa nyumba 560 Kawe Jijini Dar es Salaam.
Na Munir Shemweta, WANMM
0 Maoni