Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Angeline
Mabula, amewataka wamiliki wa ardhi nchini kuhakikisha wanalipa kodi ya pango
la ardhi kwa wakati ili kuepuka kutozwa riba ya malimbikizo ya kodi hiyo.
Dkt. Mabula alisema hayo wilayani Ngara mkoa wa Kagera
wakati akikabidhi hati miliki za ardhi kwa wananchi wa wilaya hiyo wakati wa
ziara yake mkoani Kagera.
Aliwataka wamiliki wa ardhi nchini wanaopatiwa hati milki
kuendelea kulipa kodi ya pango la ardhi kila mwaka na kubainisha kuwa, iwapo
mmiliki atapitisha mwaka mmoja bila kulipa kodi basi atalazimika kulipa kodi
inayoambatana na riba.
‘’Kila mwaka wewe kalipe ili uwe mteja mzuri wa serikali,
katika ardhi uliyo nayo usilimbilize madeni maana mwisho wa siku utakuja
kushindwa na kuanza kushitakiana na serikali kwenye Baraza la Ardhi na Nyumba
la wilaya bila sababu,’’ alisema Dkt. Mabula.
Dkt. Mabula aliongeza kwa kusema kuwa, wizara yake
imeboresha huduma zake kutoka analogia kwenda digitali unaowezesha taarifa za
wamiliki wa ardhi kuwa katika mfumo wa kieletroniki na kurahisisha taratibu za
utoaji hati.
‘’Kwa sasa utendaji wa wizara umebadilika sana ambapo
mmiliki wa ardhi anayeomba kumilikishwa anaweza kupata hati ndani ya muda mfupi
iwapo atakuwa amekabilisha taratibu zote za umiliki,’’ alisema Dkt Mabula na
kuongeaza.
‘’Kwetu sisi huku ambapo mifumo ya kidigitali haijakaa sawa
mwombaji hati anaweza kuchukua mwezi moja ama miwili lakini kwa kule ambapo
mifumo ya kidigitali ishaanza kutumika basi inaweza kabisa kuchukua hati ndani
ya wiki moja’’.
Vile vile, Waziri wa Ardhi alisema kuwa, kupitia maboredsho
ya huduma za sekta ya ardhi hivi sasa wamiliki wa ardhi wanapokea bili za kodi
ya pango la ardhi kupitia simu zao za mkononi.
Wananchi waliopokea hati zao wameipongeza wizara ya ardhi
kwa kufanya maboresho yatakayosaidia wamiliki wa ardhi kupata hati kwa muda
mfupi sambamba na kupata bili za kodi kupitia simu zao za mkononi.
Mkazi wa Ngara Godfrey Niyonzima ameshukuru kwa kupatiwa
hati na kukabidhiwa na Waziri mwenye dhamana ya Ardhi hasa baada ya
kuzihangaikia kuzipata hati hizo kwa takriban miaka sita.
‘’Kwanza nishukuru kwa kufanikisha kupata hati zangu sita za
ardhi lakini pia niipongeze wizara ya ardhi kwa kufanya maboresho ambayo naweza
kusema yanakwenda kurahisisha upatikanaji hati pamoja ulipaji kodi ya pango la
ardhi,’’ alisema Niyonzima.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline
Mabula amemaliza ziara yake mkoani Kagera na anatarajia kuendelea na ziara zake
katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Mbeya, Njombe, Iringa na Morogoro.
Na Munir Shemweta, WANMM NGARA
0 Maoni