Wapiga Kura 74,642 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 13 za Tanzania Bara kesho Julai 13, 2023.
Jumla ya wapiga kura 74,642 walioandikishwa kwenye Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi huu mdogo na jumla
ya vituo 205 vya kupigia kura vitatumika.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele katika Risala ya Uchaguzi huo mdogo unaofanyika
kujaza nafasi wazi za udiwani.
Jaji wa Rufaa Mwambelegele amewataka wasimamizi wa uchaguzi,
vyama vya siasa na wagombea kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi
wakati wa Uchaguzi Mdogo wa madiwani katika Kata 13 za Tanzania Bara.
Uchaguzi huo mdogo utashirikisha, Kata ya Ngoywa katika Halmashauri
ya Wilaya ya Sikonge, Kata ya Kalola katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui
mkoani Tabora na za Sindeni katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Potwe
katika Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Kwashemshi katika Halmashauri ya Wilaya
ya Korogwe na Bosha katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga zote za Mkoa wa
Tanga.
Kata nyingine ni Mahege katika Halmashauri ya Wilaya ya
Kibiti mkoa wa Pwani, Kata ya Bunamhala katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi,
mkoa wa Simiyu, Kata ya Njoro na Kalemawe zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya
ya Same mkoani Kilimanjaro, Kata ya Kinyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Makete
mkoa wa Njombe, Kata ya Magubike katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa mkoa wa
Morogoro na Kata ya Mbede katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe mkoa wa
Katavi.
Aidha, amevitaka vyama vya siasa, wagombea na wadau wa
uchaguzi kuepuka kujihusisha na matukio yenye viashiria vya uvunjifu wa amani
kwani jukumu la kulinda amani ni la kila mmoja, hivyo wahakikishe wanalinda
amani iliyopo nchini.
“Jukumu la kulinda amani ya nchi yetu ni la kila mmoja wetu
wakiwemo wananchi, vyama vya siasa, wagombea na wadau wengine wa uchaguzi,” alisema
Jaji wa Rufaa Mwambegele.
Aliongeza kuwa Sheria na Kanuni za Uchaguzi zimeweka mamlaka
na taratibu zinazotakiwa kufuatwa iwapo kutakuwepo na malalamiko yoyote wakati
wa uchaguzi, hivyo amevitaka vyama vya siasa na wagombea kufuata taratibu hizo
ili uchaguzi huo ufanyike kwa uhuru na haki.
Mweyekiti huyo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi amewataka wapiga
kura wote waliojiandikisha katika Kata 13 za Tanzania Bara kujitokeza kupiga
kura ili waweze kuwachagua madiwani wanaowataka.
Amevitaka vyama vya siasa wagombea na wafuasi wao kuzingatia
kuwa kampeni za uchaguzi zinakamilika leo Julai 12,2023 saa 12:00 jioni hivyo
hawaruhusiwi kufanya mikutano ya kampeni kuanzia muda huo na hawaruhusiwi
kutumia alama za vyama zinazoashiria kampeni kama vile vipeperushi, bendera na
mavazi.
Pia, Jaji Rufaa Mwambegele
amevikumbusha vyama vya Siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi huo, kuzingatia
wajibu wao wa kuweka mawakala katika vituo vyote vya kupigia, kuhesabu na
kujumlishia kura.
“Upigaji kura utafanyika katika vituo vile vile vilivyotumika
wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa
1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni. Iwapo watakuwepo wapiga kura katika
mstari ambao walifika kabla ya saa 10:00 jioni na hawajapiga kura, wataruhusiwa
kupiga kura, mtu yeyote hataruhusiwa kujiunga katika mstari wa wapiga kura
baada ya saa 10:00 jioni,” alisema Jaji Rufaa Mwambegele.
Aliongeza “Tume kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 62(1)
cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura 292, imeruhusu wapiga kura
ambao wamepoteza kadi zao au kadi kuharibika kutumia vitambulisho mbadala”.
Amevitaja vitambulisho mbadala kuwa ni Passi ya Kusafiria,
Leseni ya Udereva au Kitambulisho cha Uraia kinachotolewa na Mamlaka ya
Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Mpiga kura aliyepoteza kadi au kadi yake kuharibika
ataruhusiwa kutumia kitambulisho mbadala iwapo tu atakuwa ameandikishwa kwenye
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na jina lake lipo kwenye orodha ya wapiga kura
kwenye kituo anachopigia kura.
Mwambegele amekumbusha kuwa katika vituo vya kupigia kura
kipaumbele kitatolewa kwa wagonjwa, watu wenye ulemavu, wazee, wajawazito na
akina mama wanaonyonyesha watakaokuwa na watoto vituoni na kutakuwa na majalada
ya nukta nundu katika vituo vya kupigia kura kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa
kuona ili weweze kupiga kura wenyewe. Alifafanua kuwa kwa wapiga kura wenye
ulemavu wa kuona ambao hawawezi kutumia majalada hayo wanaruhusiwa kwenda
vituoni na watu watakaowachagua wenyewe kwa ajili ya kuwasaidia kupiga kura.
Jumla ya vyama vya siasa 17 vimesimamisha wagombea katika
uchaguzi huo mdogo ambapo Tume imevipongeza vyama hivyo na wagombea wao kwa
kutumia haki yao ya msingi ya kikatiba kujitokeza kushiriki katika uchaguzi huo
mdogo wa Udiwani.
Na Mwandishi Maalum - NEC
0 Maoni