Waziri wa Maliasili na Utalii wa Tanzania, Mhe. Mohamed
Mchengerwa, ataliwakilisha Bara la Afrika katika nafasi ya Makamu wa Rais
kwenye Baraza Kuu (General Assembly) la Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii
Duniani (UNWTO).
Tanzania imepitishwa kwa kauli moja jana , katika Mkutano wa UNWTO Kanda ya Afrika kuliwakilisha Bara la Afrika na
nafasi hiyo ya Tanzania itathibitishwa rasmi kiutaratibu tu (formality) kwenye
Mkutano Mkuu wa UNWTO Oktoba mwaka huu mjini Samarkand, nchini Uzbekstan.
Kwa nafasi hiyo Waziri Mchengerwa atakuwa Makamu wa Rais wa
Baraza hilo linalofanya maamuzi mengi makubwa duniani kuhusu utalii kwa niaba
ya Umoja wa Mataifa (UN) kwa kipindi cha miaka miwili.
Muda mfupi uliopita tena majira ya saa tatu usiku huu nchini
Mauritius Tanzania imeshinda tena nafasi nyingine muhimu katika UNWTO ya Ujumbe
wa Kamati ya Utendaji ya Baraza Kuu. Kamati hiyo ndiyo huchambua Bajeti na
miradi ya kutekelezwa kabla haijapelekwa kwenye Baraza Kuu la UNWTO.
Nchi 13 za Afrika ziligombea nafasi hiyo ya utendaji na
zilitakiwa 6, ambapo katika kura zilizopigwa Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi
sita zilizopata kura nyingi na sasa, kiutaratibu tu tene, zitaidhinishwa katika
Mkutano wa Oktoba, 2023.
Katika hatua nyingine mwishoni mwa Mkutano huo Tanzania
imeng’ara tena kwa kuchaguliwa kuwa miongoni mwa Wajumbe wa Kikosikazi cha
Kuitangaza Afrika (Rebrand Africa Working Group).
0 Maoni